Mechi za kundi C na kundi D zinaanza leo katika viwanja vinne vya miji minne tofauti hapa nchini Brazili.
Mchezo wa mapema umeanza mishale ya saa 7.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ukizikutanisha timu kutoka bara la Amerika ya Kusini, Colombia na timu kutoka bara la Ulaya , Ugiriki. Mtanange huu utapigwa katika kiwanja cha Estadio Mineirao katika mji wa Belo Horizonte.
Mchezo wa pili kwa siku ya leo utapigwa katika dimba la Estadio Castelao mjini Fortaleza wakati mataifa mawili kutoka katika bara la Amerika Kusini, Uruguay na Costa Rica watamenyana. Mchezo huo utapigwa saa 10.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Mchezo wa tatu ni mchezo ambao unasubiriwa na wengi, mchezo kati ya Uingereza na Italia utakaopigwa saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki katika dimba la Arena Amazonia mjini Manaus.
Mchezo wa kufunga ratiba ya leo ni mchezo kati ya timu kutoka barani Afrika, Ivory Cost na timu kutoka barani Asia, Japani na utapigwa muda wa saa 4.00 alfajiri katika dimba la Arena Pernambuco mjini Recife.