RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Mainzi ni kama ameridhia mchakato wa uchaguzi wa Simba SC uendelee, lakini tu ameshindwa kuweka wazi.
“Kwa ustawi wa soka ya Tanzania, naamini maelewano yatapatikana,”amesema Malinzi akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo, makao makuu ya TFF, makutano ya mitaa ya Garden na Ohio, Dar es Saalaam.
Waandishi wa Habari walitaka kujua kama ameruhusu zoezi la uchaguzi wa Simba SC, liendelee au la kufuatia kauli ya Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa klabu hiyo, Alhaj Ismail Aden Rage juzi.
![]() |
Rais Malinzi akizungumza katikati |
“Namshukuru Mwenyekiti wa Simba SC, Rage na Kamati yake ya Utendaji tangu juzi wamekuwa katika mawasiliano na mimi kwa nia nzuri tu, wakiomba uchaguzi usisimamishwe. Nami nimeruhusu mgombea mmoja aliyekata rufaa yake Kamati ya Rufani ya TFF, kesi yake isikilizwe leo.
Mazungumzo yanaendelea, na yataendelea baada ya kikao cha leo, naamini hakuna kitakachoharibika, ufumbuzi utapatikana,”amesema Malinzi.
TFF ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Simba SC hadi hapo klabu hiyo itakapounda Kamati ya Maadili ambayo itasikiliza masuala ya kimaadili kuelekea uchaguzi huo.
Malinzi alisema mwishoni mwa wiki kwamba Simba SC inatakiwa kuwa imekwishaunda Kamati ya Maadili hadi kufika Juni 30, mwaka huu, hatua ambayo alidai imefuatia TFF kupokea malalamiko mengi juu ya ukiukwaji wa maadili kwa baadhi ya wagombea na wanachama wa klabu hiyo.
Malinzi alisema kwamba baada ya kuundwa kwa Kamati hiyo Maadili itasikiliza malalamiko yote ya kimaadili yanayougubika mchakato wa udhaguzi huo, ambao awali ulipangwa kufanyika Juni 29, mwaka huu.
Aliagiza kwa sasa Kamati ya Utendaji ya Simba SC iliyopo madarakani chini ya Mwenyeiiti wake, Rage itaendelea kuiongoza klabu hiyo hadi hapo mchakato wa uchaguzi utakapokamilika.
Lakini mwanzoni mwa wiki, Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC ilimpinga Malinzi, ikisema TFF haina mamlaka ya kusimamisha uchaguzi huo na Jumatatu, Rage akamuomba raisi huyo wa TFF aache mchakato wa zoezi hilo uendelee kwa manufaa ya Simba SC