
Mtu tagemeo: James Rodriguez alifunga mabao mawili na kuonesha kiwango cha hali ya juu.
JAMES Rodriguez, kijana mwenye miaka 22, mwenye thamani ya paundi milioni 37.5 amekaa juu ya wafungaji, Lionel Messi, Muller na wengine na kuwa mshambuliaji anayeongoza kwa mabao mengi katika kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil akiwa amefikisha mabao matano.
Haikuwa rahisi kwa kijana huyu mdogo kufanya maajabu katika fainali zinazoendelea Brazil hasa hatua ya makundi na hatua ya 16.
Rodriguez jana amefunga mabao mawili na kuisaidia Colombia kuitandika Uruguay mabao 2-0 na kufuzu hatua ya robo fainali.
Alifunga mabao hayo katika dimba la Maracana na kuwanyanyua mashabiki wa Colombia waliokuwa na matumaini na mashujaa wao.
Bao la kwanza lilikuwa bora sana baada ya kuachia shuti kali ambalo linaonekena kuwa miongoni mwa mashuti bora katika mashindano haya na mashindano mengine yaliyowahi kufanyika.
Bao la pili alimalizia kazi nzuri ya mchezaji mwenzake na kuivusha Colombia hatua ya robo fainali ambapo Ijumaa ya wiki ijayo watacheza na wenyeji wao Brazil.

Shuti la ajabu: Rodriguez alivunja ngome ya Uruguay na kutandika shuti matata nje ya boksi na kufunga bao la kuongoza.

Namba 10 kamili: Rodriguez aliivusha Colombia hatua ya robo fainali na kuonesha kiwango ambacho hawajawahi kucheza kombe la dunia.

Mfalme wa kucheza: Rodriguez na Los Cafeteros wakishangilia bao lao kwa kucheza kwa staili moja.