Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuna mambo ya hovyo ambayo yapo ndani ya Chama cha Mapinduzi ambayo yanahitaji kuhojiwa na kupatiwa majibu yenye tija.
Aikihutubia maelfu ya wananchi jana waliojitokeza kumsikiliza katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza Dkt. Magufuli alisema anafahamu kwamba ndani ya CCM kuna mambo ya hovyo na mfano ni uwanja wa CCM Kirumba na majengo mengine ya CCM ambayo ukiuliza maduka na ofisi zinazozunguka majengo hayo mapato yake yako wapi huwezi kupata majibu ya kuridhisha.
“Ninyi wananchi wa Mwanza na wanachama wa CCM hojini haya na atakayewauliza mwambieni ni mimi Mwenyekiti wa CCM nimesema muwaulize, nataka chama ambacho mali zake zinajulikana kwa sababu ukienda kuwauliza mnakusanya shilingi ngapi kwa chumba kimoja wanaweza kukuambia ni elfu 50 kumbe wanaingiza laki 5” Alisema Rais Dkt. Magufuli
Rais Magufuli alisisitiza kwamba anaitaka CCM ya Rais wa kwanza wa Tanzania Mwl. Julius Nyerere siyo CCM ya watu ambao mchana wapo CCM na usiku wapo vyama vingine, wanaofanya hivyo ni bora wahamie huko moja kwa moja.
Aidha katika hatua nyingine Rais Dkt. Magufuli ameagiza uongozi wa Jiji la Mwanza kutowatoza ushuru wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwa wanatakiwa wanufaike na taifa lao na pia wamachinga waachwe mjini kwanza hadi hapo watakapo andaliwa mazingira mazuri ya kufanyia biashara yatakayokuwa na wateja.