
Dodoma, Julai 2022: Benki ya Stanbic Tanzania imezindua huduma mpya iitwayo Hekima Banking ambayo inawalenga wastaafu na wanaokaribia kustaafu. Hekima Banking ni huduma ambayo inakidhi mahitaji ya kipekee ya wateja lengwa ikiwa ni pamoja na kufanya miamala, akiba na uwekezaji, huduma hii inakusudia kuwapa wastaafu amani na utulivu wakati pesa zao zikiwafanyia kazi.
Huduma hiyo ambayo ilizinduliwa mjini Dodoma na, Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Jenista Joackim Mhagama inatoa fursa mbalimbali kwa mstaafu kama, kufungua akaunti ya muamala yenye riba yani Hekima Account, uwezeshaji wa bima, mafunzo ya kifedha kupitia Stanbic Financial Fitness Academy, upatikanaji wa ushauri kutoka kwa mshauri mahushi wa kifedha kwa ajili ya watumiaji wa huduma hii mpya.
Hekima Banking ni sehemu ya juhudi za Benki ya Stanbic kukuza ushirikishwaji wa kifedha kwa kuwawezesha wastaafu kuendelea kupata kipato ili waendele kuwa na uhuru wa kifedha, pamoja na kuboresha na kudumisha ubora wa maisha yao.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Wateja Warejareja wa Benki ya Stanbic, Omari Mtiga alisema, ”Tumeondoa ugumu wa kupata huduma za kibenki kwa wastaafu kwa kuwaruhusu wateja kuelewa jinsi fedha zao zinavyoweza kuwahudumia kwa urahisi na kuwawezesha kudhibiti mustakabali wao wa kifedha hapo baadae. Hekima inatoa huduma zaidi ya shughuli za miamala tu. Tunakupa zana za kusimamia vizuri pensheni yako ili kuhakikisha kuwa unaweza kukidhi mahitaji yako yote ya kifedha na ya familia yako’’.
Ikiwa na uelewa mkubwa wa mahitaji ya wastaafu, Stanbic imejitolea kuhakikisha kwamba wateja wake wanafurahia kustaafu kwao, na kubadilisha dhana yakua kustaafu ndio mwisho wa maisha. ‘’Kustaafu kwako kazi hakupaswi kumaanisha kustaafu kwa malengo na ndoto zako. Tunaongozana na wewe katika safari yako ya kustaafu vizuri kwa sababu tunaamini unaweza kufikia ndoto na matarajio yako hata wakati wa kustaafu,” aliongeza Mtiga.
Kwa upande wake Mhe. Mhagama aliipongeza Benki ya Stanbic kwa kuwapatia ufumbuzi wastaafu,na kwa kutambua umuhimu wa kutoa mafunzo ya fedha na uwekezaji kwao kwani kwa kuwapatia elimu hiyo wastaafu sasa watakuwa na zana na maarifa yatakayowawezesha kuendelea kudumisha maisha bora.
Uzinduzi wa hafla hiyo ulianza na semina ya elimu ya fedha kutoka Benki ya Stanbic Tanzania na mafunzo ya bidhaa za bima kutoka Strategies, ili kuwapa washiriki wa semina ujuzi wa kifedha na utambuzi wa huduma mbalmbali za bima.
Mteja anaweza kufungua akaunti ya Hekima kwa Shilingi 10,000 katika tawi lolote la Benki ya Stanbic au kwa kupiga simu kwenye kituo chetu cha mawasiliano kwa kujaza fomu ya kufungua akaunti na kutoa pasipoti ya kusafiria au kitambulisho cha NIDA na picha moja ya pasipoti.
Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka NSSF, Strategis, wateja wa Benki ya Stanbic na wafanyakazi wa benki ya Stanbic.
…MWISHO…