Sarafu mpya inaweza kutumika katika baadhi ya maduka
Benki kuu ya Zimbabwe imezindua sarafu za dhahabu katika juhudi za kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei huku kukiwa na mdororo wa sarafu ya nchi hiyo.
Kiwango kikuu cha riba cha benki kuu kiliongezeka zaidi ya mara mbili mwezi huu hadi 200% baada ya kiwango cha mfumuko wa bei kupanda zaidi ya 190%.
Kila sarafu itawekwa bei kwa kiwango cha soko la kimataifa kwa wakia moja ya dhahabu pamoja na 5% kwa gharama za uzalishaji.
Kufikia Ijumaa, wakia moja ilikuwa na thamani ya takriban $1,724 (£1,435).
Itawezekana kutumia sarafu hizo madukani, ikiwa zitakuwa na chenji ya kutosha, kulingana na gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe, John Mangudya.
Sarafu hiyo inaitwa ‘’Mosi-oa-Tunya’’ ambayo ina maana ya ‘’Moshi Unaounguruma’’ na inarejelea Maporomoko ya maji ya Victoria, kwenye mpaka kati ya Zimbabwe na Zambia.
Source: BBC SWAHILI