
Naibu Katibu Mkuu Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Grace Magembe amewashukuru wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Newala kwa kutoa eneo lenye ekari 64 kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nambunga pamoja na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Masasi kwa kutoa eneo ekari 200 kwaajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri.
Vilevile amewapongeza kwa kutoa nguvu kazi katika uchimbaji wa msingi, usimamizi wa ujenzi, usombaji wa mchanga, mawe pamoja na maji akisisitiza kuwa kwa kiasi kikubwa ushiriki wao umepunguza gharama za utekelezaji wa miradi.
Hayo yamebainishwa baada ya Dkt. Magembe kupokea taarifa na kukagua ujenzi wa kituo cha afya nambunga kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya Newala na Hospitali ya Halmshauri ya Masasi tarehe 27 Julai 2022.
Dkt. Magembe amewakumbusha Wakurugenzi wa Halmashauri hizo zote kuhakikisha maeneo hayo yanapimwa na kupatiwa hati ili kuimarisha ulinzi na usalama wa majengo yanayojengwa sasa na hata baadae.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi aliahidi kuandaa mpango kazi wa haraka wa kazi zilizobaki katika ujenzi wa wodi ya watoto, wodi ya wanaume , wodi ya wanawake pamoja na jengo la wagonjwa wa dharula utakaoanisha kazi zilizobaki na mtekelezaji wa kazi hizo na kuwasilisha mpango kazi huo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara.
Dr Magembe amemsisitiza Mkurugenzi kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Septemba 2022 ujenzi wa wodi za watoto, wodi ya wanawake pamoja na wodi ya wanaume uwe umekamilika na ifikapo tarehe 15 Agosti 2022 ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharula uwe umekamilika.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Newala amesema ujenzi wa nyumba ya mtumishi, jengo la wagonjwa wa nje ( OPD) pamoja na jengo la maabara unaotekelezwa katika kituo cha afya Nambunga utakamilika ndani ya wiki mbili tokea tarehe ya leo.

