

Waziri wa afya nchini Tanzania Mh. Ummy Mwalimu ameujuza umma kwa taarifa ihusianayo na ugojwa wa mgunda kwa kueleza yakuwa “Taarifa za ufuatiliaji wa ugonjwa huu kutoka kwa wataalam wetu walioko Mkoani Lindi zinaonesha kuwa toka tarehe 18 Julai 2022 hadi sasa hakuna mgonjwa mpya aliyeonesha dalili za ugonjwa huu. Hivyo hadi kufikia asubuhi ya leo tarehe 29 Julai 2022, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuugua ugonjwa huu nchini ni 20 na na kati yao 3 wamefariki” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema hakuna mgonjwa aliyelazwa huku wote wameruhusiwa kurudi nyumbani na wanaendelea na shughuli zao. Hii inaendana na sayansi inayojulikana kwa ugonjwa huu kuwa, ugonjwa huu unatibika kwa kutumia dawa ambazo zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.
Amesema timu ya ufuatiliaji imebaini kuwa, miongoni mwa watu waliotangamana na wagonjwa hao (contacts) hakuna aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu hadi kufikia sasa. Hii inadhihirisha pia, ni mara chache ugonjwa huu huambikizwa kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. Vilevile, wataalamu wanaendelea na utafiti wa kina kwa binadamu, wanyama na mazingira yanayowazunguka ili kubaini na kuweka mikakati ya kuudhibiti ugonjwa huu nchini.
Source: WIZARA YA AFYA TANZANIA