
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa, ametaja miradi mbalimbali itakayopelekwa katika Mji wa Mafinga ikiwamo kujengwa kwa kituo cha mauzo ya mbao.
Akitoa salamu kwa wananchi wa Mji wa Mafinga leo katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Bashungwa amesema Mji wa Mafinga upo kwenye mradi wa TACTIC wa Mji 48 ambapo umetengewa Sh.Bilioni 11.1.
“Katika fedha hizo kwa mwaka huu tumetenga fedha ili kuanza kutengeneza Master Plan ili kwa mwaka wa fedha unaofuata 2023/24, Mheshimiwa Rais ni maelekezo yako kwamba Mji wa Mafinga ungependa kwa kuwa ni wa wafanyabiashara wakubwa wa mbao, hapa Mheshimiwa Rais umeelekeza tujenge kituo cha mauzo ya mbao kwenye Kata ya Lungemba,”amesema.
Kadhalika, amesema kati ya fedha hizo Sh.Bilioni 11.1 pia itajengwa kituo cha mabasi cha kisasa katika eneo la Kinyamambo.
“Pia katika fedha hizi ambazo umeleta Mheshimiwa Rais kuna fedha za kuweka lami Kilometa 4.2 katika Mji wa Mafinga,”amesema.
Kuhusu mapato, Bashungwa amesema Mji huo umekusanya mapato kwa asilimia 127 ikiwa ni juu ya lengo walilokuwa wamejiwekea.
“Nawaomba wananchi tuwe wazalendo kuchangia maendeleo kupitia kodi ambazo tunatakiwa kuchangia ili kazi nzuri ya miradi ya maendeleo iende kwa kasi mnayoiona,”amesema.
