Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watendaji wote Serikalini kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la agizo ni kusisitiza utekelezwaji wa maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu ili kuendelea kufikisha maendeleo katika kila eneo.
Amesema hayo jana (Jumatano, Septemba 21, 2022) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yayofanyika katika ukumbi ya Kuringe, Moshi Kilimanjaro.
“Hatuna budi kuitunza amani yetu kulingana na umuhimu wake kwani amani ni tunda la upendo, utulivu, mshikamano na maridhiano.”
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika kutafuta na kudumisha amani na usalama.
“Jukumu la kudumisha amani na kuilinda amani ni ajenda ya kidunia inayomgusa kila mmoja, ili kulinda ustawi wa vizazi vya leo na kesho.”
Pia, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua na tahadhari zote zinazohitajika ili kuendelea kudumisha amani nchini.
“Serikali ya Awamu ya Sita, inafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa kwa kuweka mikakati mbalimbali ya maendeleo inayolenga kutokomeza umaskini. Umaskini ni chanzo kikubwa cha migogoro sehemu nyingi duniani kwa sababu watu wanagombania kufaidika na rasilimali chache zilizopo.”
Ameongeza kuwa kila palipo na amani, shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi kwa ujumla. “Niwasihi wananchi kuendelea kutunza na kuilinda tunu ya amani tuliyojaliwa hapa nchini”
“Ni lazima tuendelee kuilinda amani nchini kwetu, Watanzania tuendelee kudhibiti yeyote mwenye nia ya kuiharibu amani yetu. Jukumu la kuilinda amani hii ni agenda yetu sote, tuitekeleze.”

