
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kushirikiana na viongozi wa Sekta ya Elimu ili kuhakikisha thamani ya walimu na kazi za kada hiyo zinalindwa.
Kairuki ametoa maagizo hayo mnamo tarehe 9 Januari, 2023 katika Manispaa ya Morogoro wakati wa kikao kazi cha uboreshaji wa usimamizi wa Elimumsingi nchini.
Kikao kazi hicho kimelenga kuleta maendeleo makubwa ya elimumsingi ambacho kimewakutanisha wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, Maafisa Elimu Kata, Halmashauri, Mikoa, Wathibiti Ubora wa Elimu na Maafisa wa Tume ya Walimu Mkoa wa Morogoro.
“Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya shirikianeni na viongozi wa elimu katika ngazi zote kuhakikisha kuwa hadhi ya walimu inatambuliwa, wanatiwa moyo kulitumikia Taifa lao na hawadhalilishwi na mtu yeyote” amesema Kairuki.
Waziri Kairuki pia amewataka viongozi hao kuwahamasisha wazazi kuthamini kwa vitendo kazi za walimu pamoja na kushirikiana vizuri na walimu katika suala la malezi na maendeleo ya taaluma ya watoto wawapo nyumbani na shuleni.
Aidha, amewataka wahakikishe wanafunzi wanapata umahiri wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu wamalizapo darasa la kwanza, na kwamba ufundishaji wa somo la kiingereza unaimarishwa kwa shule za msingi na Sekondari.
Amewataka viongozi wa elimu ngazi ya shule, kata, halmashauri na mikoa kuhakikisha wanafuatilia ufundishaji wa walimu darasani pamoja na kutatua kero za walimu kwenye maeneo yao ya kazi badala ya kukaa maofisini.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amewataka Wakuu wa Mikoa kuendelee kuhamasisha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi ili kuhakikisha malengo ya uandikishaji waliyokuwa wamejiwekea yanafikiwa.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa amesema katika utekelezaji wa Mradi wa BOOST kwenye eneo la uandikishaji wa wanafunzi, mpaka sasa Mkoa umeandikisha wanafunzi 65,786 wa darasa la awali wakiwemo wavulana 32,543 na Wasichana 33,243 sawa na aslilimia 93.
Amesema kwa darasa la kwanza walioandikishwa ni 74,578, kati yao wavulana ni 37,342 na wasichana ni 37,578 sawa na asilimia 94.5 wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Idara ya Elimu, Bw. Vicent Kayombo amesema katika kuboresha elimu nchini, Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa magari kwa Wathibiti Ubora wa Shule, pikipiki na posho ya Uongozi kwa Maafisa Elimu Kata ili kurahisisha Ufuatiliaji na Usimamizi wa elimu kwenye maeneo yao.
