
Akikagua Miradi hiyo chuoni hapo ambayo imegharimu jumla ya sh. bilioni 1, Januari 06, 2023 Waziri Gwajima amekipongeza Chuo hicho kwa usimamizi mzuri na kuhakikisha Miradi inakwisha kwa wakati na baadhi yake kuanza kutumika
Miradi hiyo ni pamoja na darasa la kompyuta na ofisi, ukumbi mpya wa mihadhara unaochukua wanafunzi 450 na ukumbi pacha za mihadhara zinazochukua wanafunzi 350 kila mmoja.
Hata hivyo Waziri Gwajima amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha ajenda za maendeleo kwenye jamii kwani vyuo hivyo vina nafasi kubwa ya kubadili fikra za wananchi katika masuala mbalimbali na kutatua changamoto zilizopo ikiwemo ukatili wa kijinsia na kwa watoto ikiwemo wale wanaoishi mitaani na wanaopata mimba za utotoni.
“Dhana ya ushirikishwaji wa wananchi ni muhimu katika kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii ndiyo sababu, Wizara iliamua kuzianzisha ili iwe mbinu ya kufikia Maendeleo hivyo vyuo hivi vina mchango mkubwa eneo hili” amesema Waziri Gwajima.
Aidha, Waziri Gwajima ametoa wito kwa wahitimu wote katika fani ya uanagenzi wafuatiliwe na kuunganishwa na fursa za mikopo zilizopo ili watumie taaluma hiyo kuisaidiia Jamii kwa kujiajiri na kuajiri wengine.
