Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka Viongozi mbalimbali walioteuliwa Serikalini kufanya maamuzi badala ya kuwa Watu wa kulalamika huku akisisitiza kuwa watachukua hatua kwa wale ambao wataonekana hawaendi sawa na Chama kinavyotaka.
Katibu Mkuu Chongolo ameyasema hayo leo January 24, 2023 Jijini Dodoma wakati wa mapokezi ya Wajumbe wa Sekretarieti mpya ya CCM Taifa ambapo amesema wanashangaa kuona baadhi ya Viongozi wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Viongozi wengine wanalalamika kutopewa ushirikiano na Watumishi wa chini yao, hivyo amewataka wajitathmini wao wenyewe kama wanatosha kwenye nafasi hizo.