
Akizungumza wakati wa Bonanza hilo, Waziri Mkuu ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi amesema kuwa bonanza hilo limefana sana na kama kuna mapungufu ni kidogo ambayo hata hivyo yatafanyiwa kazi ili bonanza lijalo liwe bora zaidi.
“Nakupongeza sana Mheshimiwa Spika kwa kubuni wazo la kuwa na bonanza na kulitekeleza. Limefana sana na kwa kuwa ndio linaanza naamini Bonanza lijalo litakuwa bora zaidi,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha Waziri Mkuu amewaasa Waheshimiwa Wabunge na Watumishi wa Ofisi ya Bunge kutumia bonanza kama sehemu ya kufanyia mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya ya miili yao.
“Tunatumia muda mwingi sana kukaa wakati tunatekeleza majukumu yetu, hivyo mazoezi ya Bonanza hili yatatuweka timamu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema.
Waziri Mkuu aliongeza pia kuwa mbali na mazoezi bonanza hilo lina faida nyingine zikiwemo kujenga urafiki na kudumisha udugu miongoni mwa washiriki.
“Faida nyingine ya bonanza hili ni kukuza vipaji vya kucheza michezo mingi kwa kuwa bonanza hili linahusisha michezo mingi ambayo inatoa fursa kwa kila mmoja kushiriki,” alisema.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu aliwashukuru pia wadau mbalimbali ambao walifanikisha kufanyika kwa tamasha hilo wakiwemo Benki ya NMB ambao ndio walikuwa wadhamini wakuu wa bonanza la siku ya leo.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo, Spika wa Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson aliwashukuru na kuwapongeza wote walioshiriki katika tamasha hilo.
Aidha alisema bonanza hilo limeanza vizuri na kwamba changamoto ndogo ndogo zilijitokeza zitafanyiwa kazi kwa ajili ya kufanikisha mabonanza bora zaidi.
“Bonanza hili limeonesha ya kwamba tuna uwezo wa kufanya mazoezi na pia kuwahamasisha wanananchi kufanya hivyo,” alisema.
Mbali na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watumishi wa Bunge, bonanza la leo pia lilihusisha wawakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Bonanza la Bunge la kimichezo la leo lilihusisha michezo takribani 19 ambapo kwa kiasi kikubwa Waheshimiwa Wabunge waliibuka washindi katika michezo hiyo na hivyo kuchukua vikombe vingi pamoja na Kombe la ushindi ambalo Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Mheshimiwa Festo Sanga alikabidhiwa na Waziri Mkuu.
Bonanza hilo limepangwa kufanyika mara nne kwa mwaka ambapo bonanza lijalo linatarajiwa kufanyika tarehe 24 Juni, 2023. Kauli Mbiu ya Bonanza la leo ilikuwa: Shiriki Michezo Tujenge Taifa Lenye Afya.

