Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe, Dkt. Selemani Jafo amesema biashara ya kaboni itasaidia kuleta fursa nyingi hapa nchini na kusaidia kuhifadhi mazingira.
Amesema hayo mara baada ya hafla ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya uhusiano kati ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Kampuni ya Blue Carbon kutoka Dubai.
Hafla hiyo imeshuhudiwa na Mwanamfalme wa Dubai ambaye pia ni Mwenyekiti wa kampuni ya Blue Carbon Mhe. Sheikh Ahmed Dalmook Al Maktoum na Waziri Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana.
Dkt. Jafo amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa makubaliano hayo baada ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kukamilisha uandaaji wa kanuni na mwongozo wa biashara ya kabini Oktoba 2022.
Amesema hatua ya kusainiwa kwa makubaliano hayo itafungua milango kwa wananchi kupanda miti kwa wingi na kutunza mazingira ili iweze kuingia kwenye biashara hiyo.