Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC), ambao ulitakiwa uwasilishwe leo Alhamis 9, 2023 bungeni umekwama kwa mara nyingine.
Muswada huo unakwama wakati ambao, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekuwa akiunadi kwa wadau wa sekta ya afya wakiwemo viongozi wa dini na waandishi wa habari ili kupata maoni yao kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Hii ni mara ya pili kwa muswada huo kukwama tangu usomwe kwa mara ya kwanza bungeni katika mkutano wa nane wa Bunge na kupelekwa katika kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuchambuliwa.
Mkutano wa tisa wa Bunge, muswada huo ulipangwa kujadiliwa kwa siku moja Novemba 12 mwaka jana lakini ulikwama.
Akitoa ufafanuzi kwa nini haukuwasilishwa muswada huo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema muswada huo ulishindwa kusomwa mara ya pili kwa sababu Serikali na Bunge bado walikuwa wakiendelea na majadiliano.
“Sasa hati hii haitawasilishwa leo mezani kwa sababu Bunge pamoja na Serikali tunaendelea na mashauriano juu ya mambo ambayo hatujaafikiana vizuri,” alisema.
Dk Tulia alisema Bunge lilikuwa likiendelea na mashauriano katika hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa na wabunge, wadau mbalimbali waliojitokeza katika kamati na nyingine Serikali.
Hata hivyo, Januari 20, 2023 Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo alisema kazi ya uchambuzi wa muswada huo ilikuwa imekamilika.
Credit; MWANANCHI