
Uasi wa Azimio pia unatokana na kile ambacho Odinga alidai ni “ushuru uliovuka mipaka ambao Wakenya wanatozwa na serikali unaoua biashara, kufanya familia kuwa masikini na kuharibu nafasi za uwekezaji”.
“Utozwaji wa ushuru huu ni lazima ukome ili uchumi wa Kenya uweze kufufuka kwa sababu hii, lazima serikali ya Ruto iondoke mamlakani,” alisema.
Katika uasi huo ambao Bw Odinga aliashiria utafikia kilele Machi 20, 2023, Azimio italalamikia uagizaji wa chakula kilichobadilishwa kisayansi (GMO) ambao alisema ni mpango wa kuharibu uchumi wa eneo linalokuza chakula nchini na kufanya Wakenya kuwa watumwa wa kampuni kubwa za Amerika.
Aidha, uasi huo utalenga kusitishwa kwa mchakato wa kuajiri makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ulioanzishwa na Rais Ruto huku Bw Odinga akisisitiza kiongozi wa nchi anajipanga kuiba uchaguzi mkuu wa 2027.
Alipotoa makataa ya siku 14 kwa Rais Ruto mnamo Februari 22, Bw Odinga alitaka sava ambazo IEBC ilitumia katika uchaguzi mkuu wa 2022 kufunguliwa ili kubaini ukweli wa aliyeshinda, takwa ambalo Rais Ruto alikataa kutimiza.
Bw Odinga sasa anahimiza wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uasi na maandamano akisema ana hakika Rais Ruto alishirikiana na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC kumpokonya ushindi.
“Kwa kuiba kura na kupindua ushindi wa watu na kukataa kufungua sava kujua ukweli, ni lazima Ruto aende,” alisema.
Uasi huo, akaeleza Bw Odinga, pia unatokana na kunyanyashwa kwa makamishna wanne wa IEBC Juliana Cherera, Irene Marsit, Justus Nyang’aya na Francis Wanderi kwa kukataa matokeo yaliyoonyesha kwamba, William Ruto alishinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Azimio pia inalaumu Rais Ruto kwa ‘kuteka na kudhibiti’ Mahakama na Bunge na kunyima asasi za serikali uhuru zinazopatiwa na katiba, kupalilia ukabila katika uteuzi wa nyadhifa kuu serikalini na kubuni ofisi kinyume cha katiba ili kuwazawadi wandani wake na familia zao na kugawanya nchi kwa misingi ya kidini.
Azimio ilifufua madai iliyotumia wakati wa uchaguzi mkuu ya unyakuzi wa mashamba na kutoweka kwa mashahidi wa kesi iliyomkabili Ruto katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu uhalifu (ICC) kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2008.
Walilaumu Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kudai serikali ya Kenya ni kampuni na wenyehisa ni walioipigia kura.
“Tunaanza kwa kuambia Ruto na Gachagua kwamba, sisi ndio wenyehisa wa kweli kwa nchi hii, watu wote wa Kenya ni wenyehisa wa nchi yetu na hatuwezi kuvumilia serikali haramu.
Akaendelea: “Ni wakati wa vitendo, tujitokeze wote, popote tulipo ili sauti zetu zisikike na kuheshimiwa na baada ya kufanya tutakachofanya kokote katika kila kona ya nchi, tutakusanyika Nairobi kwa maandamano makubwa Machi 20 2023,” akatangaza Bw Odinga ambaye aliwasilisha salamu kutoka Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.