Waziri wa maji Jumaa Aweso akiwa ziarani Same amesema kuwa mradi wa Mwanga, Same hadi Korogwe utakamilika kwa kipindi cha miezi kumi na nne na sio kumi na nane kama Mkandarasi alivyo omba kwani Wananchi wana uhitaji mkubwa wa huduma ya maji safi na salama.
Hivyo waziri huyo amewataka wakandarasi wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe kukamilisha kazi zilizosalia katika mradi huo ndani ya miezi 14.
Ametamka hayo wilayani Same wakati wa kusaini makubaliano ya kuhuisha mkataba kati ya Wizara ya Maji na mkandarasi kampuni ya M.A. Kharif & Sons kuhusu kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
“Baada ya dhiki ni faraja, na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha za kutosha kumaliza kazi hii” Mhe. Aweso amesema na kusisitiza mkandarasi asiweke sababu zozote za kukwama mradi
Amesema wananchi wamesubiri sana maji, sasa ndani ya miezi 14 lazima wapate majisafi, salama na toshelevu.
Amesema viongozi wa Wizara watafanya kazi usiku na mchana, na kumwelekeza mkandarasi kuweka ratiba ya mpango kazi hadi kukamilisha mradi.
Akiongea kuhusu kazi zilizobaki, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema ni pamoja na kazi ya ulazaji mabomba ambayo yameshafika na kazi inaendelea.
Amesema pia, kuweka mfumo wa umeme ili kusukuma maji kwenda katika matanki, ambapo mradi una idadi ya matanki saba ya kuhudumia wananchi.
Hafla hiyo imehudhuria na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Nurdin Babu ambaye amewataka wananchi kushiriki katika miradi ya maji kwa kulinda vyanzo vya maji.
