WIZARA ya Afya imesema inafuatilia ugonjwa usiojulikana uliotokea mkoani Kagera na kuua watu watano baada ya watu saba kupata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya miili yao na Figo kushindwa kufanya kazi, ambapo wawili wako hospitali.
Ugonjwa huo usiojulikana umetokea wilaya ya Bukoba vijijini katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega, ambapo inasadikiwa watu hao saba walipata dalili hizo za homa.
Hayo yamesemwa jana na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu akizungumza na wanahabari juu ya mlipuko wa ugonjwa usiojulikana Mkoa wa Kagera. Prof. Nagu amesema kuwa jumla ya watu 7 wanasadikika walipata dalili za homa,
“Serikali imechukua hatua za kudhibiti ugonjwa huo ili usisambae kwa kuchukua sampuli kutoka kwa wagonjwa na waliofariki ili kubaini chanzo cha ugonjwa huo na ufuatiliaji wa watu wenye viashiria vya ugonjwa kwenye jamii,” – Profesa Tumaini Nagu, Mganga Mkuu wa Serikali
“Pia dawa, vifaa na vifaa tiba muhimu vipo katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Kagera na wagonjwa wanaendelea na matibabu, na elimu ya afya inaendelea kutolewa kwa jamii mkoani Kagera ili kuchukua tahadhari,”- Profesa Tumaini Nagu, Mganga Mkuu wa Serikali
“Yeyote mwenye dalili za homa, kutapika, kuharisha, kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu afike kituo cha afya, kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili, mate, machozi, damu, mkojo na kinyesi kitokacho kwa mgonjwa au yeyote mwenye dalili hizo,”-Mganga Mkuu wa Serikali