
Wanafunzi 700 raia wa India wanatarajia kurudishwa kwao kutoka Canada baada ya kugundulika kuwa walitumia barua feki za kualikwa Vyuoni ili kupata Viza mnamo mwaka 2018/19.
Watu hao wameshakabidhiwa barua za kufukuzwa nchini Canada kutoka kwa Wakala wa usalama wa mpaka wa Canada (CBSA).
Taarifa kutoka kwenye Vyombo vya habari zinasema kuwa wanafunzi hao waliomba Viza za wanafunzi kupitia kwa ofisi inayotoa huduma za Uhamiaji wa kielimu iliyopo katika mji wa Jalandhar,nchini India.
Kampuni hiyo ilimchaji kila mwanafunzi takribani dola elfu ishirini. Gharama hiyo haikuhusisha gharama za tiketi ya Ndege na amana ya usalama.
Wataalamu wanaeleza kuwa wengi wa wanafunzi hao walikwisha maliza masomo yao na kupata vibali vya kufanyia kazi na wengine kupata uzoefu wa kazi. Wakati wakijaribu kuomba vibali vya kuwa wakazi wa kudumu (Permanent Residents) ndipo walipokutwa na matatizo hayo.
Ulaghai huu wa elimu ni mkubwa na wa kipekee kuwahi kutokea nchini Canada. Wakala mmoja wa elimu mwenye uzoefu wa miaka 10 nchini India ameeleza kuwa mara nyingi ulaghai huo hufanywa kwa kughushi barua za mwaliko kutoka vyuoni na kughushi risiti za malipo ya ada nyaraka ambazo hutumika wakati wa kuomba Viza.
Baada tu ya kuingia Canada, wanafunzi hao hulazimika kwenda kusoma kwenye vyuo vingine kwani huwa hawatambuliki kwenye vyuo walivyotumia kuombea viza.