

Hatimaye wananchi wa maeneo ya Mshikamano, Msakuzi hadi Mageti wameanza kupata huduma ya Maji kwa mara ya kwanza baada ya kukamilika kwa mradi wa Mshikamano uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA).
Akitembelea maeneo ambayo yameanza kupata huduma ya maji kupitia mradi huo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amewahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa msimu huu wa sikukuu Mamlaka imewapa zawadi ya upatikaji wa huduma kwa zaidi ya asilimia 95 watafikiwa na huduma katika maeneo yao.
“Mamlaka imejizatiti kufikisha huduma kwa wananchi wote wa Dar es salaam na miji ya Mkoa wa Pwani na tunajivunia kukamilika kwa mradi huu, ambao utahudumia zaidi ya wakazi 180,000, ” alisema Kiula na kuongeza kuwa mradi umetekelezwa kwa gharama ya Tsh Bilion 4.8 zikiwa fedha za ndani za Mamlaka na kutoka mfuko maalum wa Uviko 19. 

Ndugu Ramadhan Abedi, mkazi wa Magari Saba, ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada walizochukua kuhakikisha mradi unakamilika na kutoa huduma kwa wakati.
“Nichukue fursa hii kuipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na DAWASA kwa kutufanikishia kupata huduma ya maji kwa haraka, hii sasa ni zawadi kubwa wakati huu wa sikukuu. Imetupa heshima kubwa sana.” amesema ndugu Abedi.
Mradi wa maji Mshikamano unatarajiwa kuhudumia wakazi wa maeneo ya Mshikamano, Mpiji, msakuzi, kusini na kaskazini, machimbo, majengo mpya, Dodoma, Luguruni lapaz, Mbezi Inn, magari saba, magayana, njia panda makondeni, TAKUKURU, Kwa gamba, Luguruni dampo, Luguruni KKKT, Rising star, Msakuzi supermarket, Amani street, Miti mirefu, Madafu, Kwa mfala, Chikongowe, Masaki street, Mbezi msumi, Machimbo na Mageti.