

Dar es Salaam, Tanzania April 2023 – Benki ya Stanbic na UNDP Tanzania wametangaza ushirikiano wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa mtaji na huduma za maendeleo ya biashara kwa kampuni changa na biashara ndogo na kati za Kitanzania. Ushirikiano huu, chini ya mipango yao ya Stanbic Biashara Incubator na Funguo Innovation Programme, unalenga kuboresha ubora wa huduma za maendeleo ya biashara zinazotolewa na watoa huduma tofauti na waendeshaji wa uvumbuzi kwa kampuni na biashara changa zinazoongozwa na vijana na wanawake. Vilevile, unalenga kukuza na kusaidia mazingira yatakayoruhusu kampuni hizi kustawi.
Kadhalika, ushirikiano huu unalenga kutoa mafunzo ya kiufundi, na kujenga uhusiano na wawekezaji na wafadhili na kuongeza fursa kwa kampuni changa na biashara ndogo na kati ili kuongeza vyanzo mbalimbali vya mtaji.
Utiaji Saini wa hati ya makubaliano, yaani Memorandum of Understanding ulifanyika kwenye hafla fupi iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa ubunifu na ujasiriamali, kutoka sekta ya umma, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, waanzilishi wa kampuni za kibunifu pamoja na wandishi wa habari. Kusainiwa kwa hati hii kuliashiria kuanza rasmi kwa ushirikiano huo na kuanza kwa shughuli ya kwanza ya pamoja, ambayo ilihusisha mafunzo ya siku mbili juu ya mbinu na maarifa ya kutafuta mitaji ya uwekezaji kwa kampuni changa na biashara ndogo na za kati.
Ushirikiano huu unaendana na Lengo la 17 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, ambalo linasisitiza ushirikiano kwa maendeleo endelevu. UNDP Tanzania na Benki ya Stanbic Tanzania wanatambua kuwa ushirikiano ni muhimu katika kuendeleza mfumo wa uvumbuzi na ujasiriamali wa Kitanzania, na wamejitolea kufanya kazi pamoja kukuza maendeleo endelevu kupitia ushirikiano.
Akizungumza juu ya ushirikiano huu, Bi. Christine Musisi, Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, alisema, “Tunafurahi kushirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania kukuza ubunifu na ujasiriamali nchini Tanzania. Tunaamini ushirikiano huu utatusaidia kuongeza ufikiaji wa mtaji na huduma za maendeleo ya biashara kwa kampuni changa na biashara ndogo na kati za Kitanzania, hivyo kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania, na hatimae kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.”
Vivyo hivyo, Bw. Kevin Wingfield, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, alisema, “Tunafurahi kushirikiana na UNDP Tanzania kwenye mpango huu. Kama benki, tumejitolea kuunga mkono wajasiriamali na biashara ndogo ndogo, na tunaamini kuwa ushirikiano huu utasaidia sana kuongeza ufikiaji wa mtaji na huduma za maendeleo ya biashara kwa kampuni changa na biashara ndogo ndogo na kati za Kitanzania.”
*Mwisho*