Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema hadi kufikia Machi, mwaka huu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linaidai wateja mbalimbali Sh244 bilioni.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Tauhida Cassian Gallos amehoji kuna mpango gani wa kukusanya madeni ya Tanesco katika taasisi kubwa ili Shirika hilo liweze kujiendesha.
Akijibu swali hilo leo Jumanne Aprili 25,2023, Byabato amesema mpaka kufikia Machi 2023, shirika hilo limekuwa likidai Sh244 bilioni kutoka kwa wateja wake mbalimbali.
Amesema kati ya fedha hizo taasisi za umma zinadaiwa zaidi ya Sh86 bilioni kati Sh244 bilioni.
Anesema ili kuzuia ukuaji na kuwezesha ukusanyaji wa deni, kwa upande wa Serikali, Serikali inahakikisha inatenga na kuweka fungu la fedha za kulipia huduma hii.
Katika swali ya nyongeza Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Asha Abdalah Juma amehoji ni mikakati gani Serikali inafanya kuhakikisha kuwa madeni hayo yanalipwa.
Akijibu swali hilo, Byabato amesema deni hilo ni la siku nyingi kabla ya kufungwa kwa mita za Luku na kwamba shirika hilo linaendelea kuhangaika nalo madalali wa kukusanya madeni.
Amesema wameshapata madalali mawili ambao siku nyingi wataingia mtaani kuanza kukusanya fedha hizo huku kwa upande wa Serikali wataenda Hazina.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko amehoji kwanini wateja wote wasiweke mita za kulipa kwanza kabla ya matumizi ili kuleta usawa.
Akijibu swali hilo, Byabato amesema kati ya deni hilo, taasisi za kiserikali zinadaiwa Sh86 bilioni.