Mkurugenzi wa Kituo cha Takwimu kutoka Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (UNECA), Oliver Chinganya amehimiza matumizi ya vifaa vya kisasa katika suala zima la ukusanyaji na utunzaji taarifa za takwimu nchini.
Chinyanga ameyasema hayo jana, Aprili 25,2023 wakati alipotembelea Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) kilichopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya ziara ya siku tatu itakayomkutanisha na uongozi wa chuo pamoja na wanafunzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha uongozi wa chuo hicho Chinganya alisema ubora wa takwimu unategemea na vifaa vinavyotumika kwa ajili ya kukusanyia taarifa.
Akitolea mfano zoezi la Sensa lililofanyika mwaka jana nchini anasema akiwa ni miongoni mwa walioshiriki alishuhudia matumizi ya vifaa bora na vya kisasa.
Anasema vifaa vilipelekea urahisi wa zoezi hilo hivyo amehimiza hata katika ukusanyaji wa taarifa kwa ajili ya takwimu zingine ni muhimu kuendelea kutumia vifaa hivi vya kidijitali.
“Ukusanyaji wa taarifa zamani ilikuwa wanatumia karatasi lakini hivi sasa vinatumika vifaa kama vishikwambi, mfano Tanzania ilikuwa ni nchi ya kwanza Afrika kutoa majibu ya Sensa ndani ya siku 45 pekee kutokana na matumizi ya vifaa hivyo,” alisema Chinganya.
Akizungumzia mitalaa ambayo wanafunzi wanafundishwa chuoni Chinganya aliweka wazi lazima iendane na mabadiliko ya dunia akitolea mfano matumizi ya mtandao.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Dk Tumaini Katunzi alisema ujio wa Chinganya utawanufaisha kwasababu ni mbobezi wa kimataifa wa masuala ya takwimu.
Alisema Chinganya anatarajia kuwepo kwa siku tatu chuoni hapo kwaajili ya kutoa elimu ya masuala ya takwimu kwa wanafunzi wa ngazi ya Uzamivu.