SERIKALI inakusudia kununua vivuko vidogo viwili ‘sea taxi’ vyenye uwezo wa kubeba abiria 250 kila kimoja baada ya kutumia vivuko kama hivyo vya kampuni ya Azam Marine na kuonesha ufanisi katika kuondoa ucheleweshaji wa abiria kutoka na kuingia Kigamboni.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete ameliambia Bunge wakati akijibu Swali la Mbunge wa Kigamboni Dk. Faustine Ndugulile kwamba taratibu za manunizi zinaendelea kupata vivuko hivyo kwa ajili ya Magogoni – Kigamboni.
“Tulipata wazabuni wawili hata hivyo waliweka gharama kubwa sana. Tunafanya mchakato upya kwa ajili ya kupata mzabuni,” amesema Mwakibete. Dk Ndugulile alihoji ni lini ujenzi wa kivuko kipya cha Kigamboni utaanza baada ya kutengewa fedha mwaka 2022/2023.