Mwanzilishi wa Tanzania Startuos Association (TSA), Zahoro Muhaji amesema namna nzuri ya kunzisha biashara ni kuanzia sokoni kwa kuangalia kuna uhitaji wa kiasi gani wa kile unachotaka kukiuza.
Amesema kuwa mara nyingi watu wamekuwa wakifanya biashara ambazo wana hisia nazo huku akitolea mfano wa wanawake wengi kuuza vipodozi.
Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi, Aprili 27, 2023 katika kongamano la Wafanyabiashara wachanga, wadogo na Kati (MSMEs) lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited ambalo limekutanisha wadau mbalimbali ili kujadili nini kifanyike ili kuwawezesha kufanya biashara zao kwa ufanisi.
Kongamano hilo linaelendelea katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki jijini Dar es Salaam ambalo limedhaminiwa na Ashton, benki ya CRDB, Kampuni ya Usafirishaji DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media na Ukumbi wa Mikutano wa Dome.
Muhaji amesema kuangalia mahitaji soko lilipo, linataka nini,aina gani ya bidhaa itakayomlipa na kujua mtaji kiasi gani unahitajika ni mambo muhimu katika biashara
“Kwa mfano, kila wakati wa uchaguzi kila kitu kilichokuwa na rangi ya kijani kilikuwa kinauzika kwa sababu wengi walikuwa wakitaka kuvaa nguo zao za chama anataka kumatch na wenzake na unakuta rangi fulani inanguvu hivyo soko lina nguvu ya kujua nini unataka kufanya,” amesema Muhaji.
Amesema kuwa namna nyingine nzuri ya kuanzisha biashara ni kujihusisha na watu wanaofanya biashara ikiwemo kujiunga na atamizi ili kujua wengine wanapitia changamoto gani hivyo inamuwezesha yeye kujifunza kwao na wao wanajifunza kwake.
“Mkiwa wengi ni rahisi kusogeza biashara zenu hata ule uoga unakutoka, pia kuna biashara nyingine ni vyema kwenda sehemu mbalimbali kama ushonaji ni vyema kwenda SIDO kwa sababu kuna huduma nyingi zinazopatikana ikiwemo vibali vya TBS (Shirika la Viwango Tanzania).
Amesema duniani kote biashara kubwa inamilikiwa na watu wengi jambo linaloweka urahisi katika kufanikiwa.
“Usifanye biashara ukiwa umejifungia chumbani toka na nenda kwenye atamizi angalia wengine wanafanya nini na hii itakusaidia wewe kuweza kujifunza na kufika mbali,”
Amesema baadhi ya biashara huhitaji wewe kukipenda huku akitoa rai kuwa mara zote biashara si suala la hisia.
Kongamano hilo limedhaminiwa na Ashton, benki ya CRDB, Kampuni ya Usafirishaji DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds media na Ukumbi wa Mikutano wa Dome.
CC; Mwananchi