Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Azam na sasa Singida Big Stars, Hans Pluijm ni wazi kila mmoja anajua aliwahi kuwa mwanachama wa klabu ya Yanga kwa wakati huo.
Pluijm alivyoondoka kwenda Singida United na baadaye Azam FC, wengi wao waliendelea kuamini kwamba kocha huyo bado mwanachama wa Yanga kutokana na awali kujisajili.
Kupitia mahojiano yaliofanywa na Spoti mikiki na Pluijm akiwa kwake Singida, Mtaa wa Paradise na amefunguka mengi ikiwemo suala lake la uanachama Yanga pamoja na mipango yake ya sasa akiwa na Singida Big Stars.
“Nilikuwa na kadi, lakini haikuendelea kuwa hai kwa sababu sikuwa nalipia, kwahiyo tayari mimi si mwanachama wa kule tena kwa muda mrefu sana.
“Lakini mashabiki wameendelea kuwa wema kwangu kwa sababu huwa wananitumia ujumbe wa kunisalimia nikiwa hapa na hata kabla sijaja kabisa huwa wananisalimia,” anasema Pluijm.
“Ilinishangaza sana kiukweli, mimi kwenda kwenye kile cheo nikiwa nimeifanyia vitu vingi timu, nilikuwa TD (Technical Director/Mkurugenzi wa ufundi), lakini sikuwahi kuwa hata na ofisi.
“Yanga yetu kiukweli kila mmoja anajua ni namna gani ambavyo tulikuwa, uwanja wa mazoezi ambao tulikuwa tunafanya mazoezi ni tofauti bila shaka na ambao leo hii wanafanya.
“Hata kwenye uendeshaji unaona kabisa kuna mabadiliko kwa sasa, unajua zamani pale kila mtu alikuwa anaongea ila kwa sasa kuna uongozi ambao wapo watu wa kuzungumza,” anasema kocha huyo raia wa Uholanzi.
Pluijm anasema: “Baadhi ya viongozi wanaongea sana halafu mazoezini hawaji, mimi nilikuwa na misimamo yangu kwa sababu najua mashabiki wanaipenda timu yao hivyo walikuwa wanahitaji matokeo mazuri tu na sio kitu kingine.”
“Msuva walikuwa wanamsema sana, lakini mimi nilikuwa namwambia utacheza na unachotakiwa kufanya ni kuwaonyesha kwamba unaweza kwa kuonyesha kipaji chako.
“Leo nenda kamuangalie Msuva yupo vipi, kama ningemkatisha tamaa kwa kipindi kile kwa kuamua kusikiliza nini baadhi ya watu na mashabiki wa Yanga wanataka basi ningempoteza,” anasema.