
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema zaidi ya Wagonjwa 5000 kutoka nje ya Nchi zinazoizunguka Tanzania huja kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kila mwaka kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika eneo la miundombinu, vifaa tiba na Watumishi wenye ujuzi mkubwa.
Dkt. Mollel amesema hayo alipofanya ziara na kuongea na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
Amesema “Watu wanaotoka Nje ya Nchi zinazotuzunguka kwa mwaka kuja kupata huduma za kibingwa na kibingwa bobezi ni zaidi ya 5000, kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Rais Samia katika Sekta ya Afya.”
Amesema tayari Serikali ya Tanzania imesaini mikataba na Nchi za Zambia, Malawi kwa ajili ya kuleta Wagonjwa wao nchini kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.
Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imepunguza 97% ya Wagonjwa kwenda kupata matibabu nje ya Nchi, kutokana na uwekezaji wa vifaa tiba, miundombinu pamoja na Watumishi wenye ujuzi, hivyo kuifanya Nchi ya Tanzania kuwa kimbilio la matibabu kwa baadhi ya Nchi ikiwemo Nchi zilizo majirani na Tanzania”