Serikali ya Tanzania na Canada zimepanga kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali yakihusisha shughuli za utafiti wa madini, kujenga uwezo wa wataalamu na kushirikiana katika kuhamasisha shughuli za uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji katika Sekta ya Madini. Hayo yamebainishwa na Balozi wa Canada nchini Tanzania Kyle Nunas leo Mei 8, 2023 jijini Dar es Salaam alipokutana na kuzungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali na Wataalamu kutoka Wizara ya Madini na taasisi katika kikao kilicholenga kuzungumzia shughuli za kuendeleza uchimbaji wa madini.
“Ushirikiano wa Tanzania na Canada katika sekta ya madini utaongeza tija kwenye uchumi, kuongeza ajira, kuwajengea uwezo watumishi ili kuwezesha watanzania kuzalisha madini kwa wingi ikiwemo bidhaa zinazotokana na madini hayo” Kheri Mahimbali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini
“Tunaomba tuweze kuwa na ushirikiano na Canada katika kutangaza shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika hapa nchini, tuendelee kukutana na kuzungumza mara kwa mara ili mchango wa sekta ya madini ukue katika uchumi wetu” Kheri Mahimbali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini
“Tanzania iko tayari kushirikiana na Cananda kuhakikisha Taifa linanufaika na rasilimali madini ikiwemo madini ya kimkakati ili kukuza uchumi” Kheri Mahimbali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini