Klabu ya Azam FC imetoa pole kwa Meneja wao wa Masoko na Mauzo, Tunga Ally, kwa kunusurika kwenye ajali ya gari maeneo ya Mnazi Mmoja, kilomita tano kuelekea Lindi, wakati akiwa safarini kurejea jijini Dar es Salaam akitokea Mtwara, na gari lake binafsi aina ya Nissan Patrol.
Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii Azam FC wameandika “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa kiongozi wetu huyo na baadhi ya watu wa masoko aliokuwa ameambatana nao kwenye gari hiyo yenye nambari ya usajili T 381 AYX”
Kwa mujibu wa Ally, gari hiyo ilipata hitilafu ya kukatika vishikio (studs) vya matairi mawili ya nyuma, iliyopelekea matairi hayo kuchomoka na kwa bahati nzuri aliweza kupambana na changamoto hiyo hadi gari hiyo iliposimama.
Aidha katika hatua nyingine, Azam FC imewashukuru mashabiki wa klabu ya ya Simba waliokuwa nyuma yao na basi lao aina Coaster kwa kuweza kusimama na kujumuika nao na kuwapa pole wahanga wa ajali hiyo.