JESHI la Polisi limesema litaimarisha ulinzi kabla, wakati na baada ya mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Yanga na Marumo Gallants ya Afrika Kusini iliyopangwa leo Mei 10, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Mchezo huo utaanza saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Muliro amesema katika taarifa mapema leo kuwa “baadhi ya mashabiki wenye tabia ya kuwasha fataki uwanjani, kurusha chupa au kitu chochote wachukue tahadhari.”
“Jeshi la Polisi halitavumilia tabia hizo ambazo zimeansa kuzoeleka na watakaokamatwa wakati au baada ya mchezo huo watachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Muliro katika taarifa kwa vyombo vya habari.