Wajasiriamali (Machinga) wa Visiwani Zanzibar watafurahi kufanya shughuli zao bila usumbufu kama ilivyo kwa utaratibu unaotumika Bara, kufuatiwa kuasisiwa kwa mfumo mpya wa utambuzi ambao umesajili Machinga 22,236.
Usajili huu unaenda sambamba na utoaji wa vitambulisho vitakavyowawesha kufanya biashara kwa amani na hivyo kuinua vipato vyao katika mikoa na wilaya zote za Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Masoud Ali Mohammed wakati wa kipindi cha maswali na majibu leo Mei 11, 2023 katika baraza la wawakilishi Zanzibar.
Kwa mujibu wa waziri huyo, kati ya wamachinga waliotambuliwa; 6, 085 kila mmoja ameshalipia Sh30, 000 kama ada yake ya mwaka na ndipo kupatiwa kitambulisho chake kitakachompa nafasi ya kufanya biashara bila tafulani.
Waziri Masoud alikuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Uzini Haji Shaaban Waziri akisema licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali bado baadhi ya wajasiriamali wanakabiliwa na changamoto mbalimbali na kutaka kujua hatua zaidi za Serikali zilipofikia kuwatambua wakiwemo mamalishe.
“Takwimu zinaonesha kwamba hadi kufikia Aprili 30, 2023 jumla ya wajasiriamali wadogo wadogo 22,236 wamesajiliwa na 6085 tayari wameshalipia na kupatiwa vitambulisho vyao,” amesema
Akifafanua kuhusu tozo hiyo ya Sh30, 000, Waziri Masoud amesema inajumuisha ada ya usafi na ruhusa ya kufanya biashara katika Wilaya.
“Hivyo, baada ya taratibu na kupatiwa kitambulisho cha mjasiriamali hakuna gharama nyingine yoyote ya ziada,” amesema
Amesema pia kwasasa Serikali inaendelea kujenga masoko katika Wilaya zote 11 za Unguja na Pemba kuendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara badala ya kujipanga Barabarani.