
Mhe. Majaliwa ametoa rai hiyojana Mei 10, 2023 katika hafla ya uzinduzi wa huduma za upandikizaji wa Uloto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
“Nitoe rai kwa jamii ya Watanzania kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa lengo la kufahamu afya zao na kuchukua hatua mapema.” Amesema Mhe. Majaliwa.
Ameendelea kusema kuwa, uwekezaji wa kituo hicho kinachotoa huduma ya upandikizaji wa Uloto uliofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 , huku huduma hizo zikisaidia kupunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali ili kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma hizo nje nchi.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema, huduma hii ya upandikizaji uloto ikitolewa ndani ya nchi katika Hospitali hii ya Benjamin Mkapa itagharimu shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja na kama angepelekwa nje takriban shilingi milioni 120 hadi 150 zingetumika.
Ameendelea kusisitiza kuwa, upandikizaji uloto unatoa nafuu kubwa sana kwa wagonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell) kwa kuwapunguzia kwa kiasi kikubwa maumivu na maambukizi ya mara kwa mara na wakati mwingine huwa sababu ya kupona kabisa kwa ugonjwa huu wa kudumu hivyo kutoa fursa ya wagonjwa hao kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa.
Sambamba na hilo, Mhe. Majaliwa amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imeokoa shilingi bilioni 3.5 kwa kutoa huduma ya upandikizaji figo nchini.
Huduma hiyo ilitolewa kwa wagonjwa 8 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na wagonjwa 6 kwenye Hospitali hii ya Benjamin Mkapa ambapo gharama ya kuwahudumia hapa nchini ni shilingi bilioni 1.5 ikilinganishwa na shilingi bilioni 5.0 kama wangepelekwa kutibiwa nje ya nchi, amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Hata hivyo, Mhe. Majaliwa ameilekeza Wizara ya afya kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa kuendelea kutangaza huduma hizo za upandikizaji wa Uloto ndani na nje ya nchi ili watanzania wengi wazielewe huduma hizo na ikiwezekana matangazo haya yanavuka mipaka ya nchi yetu na nchi jirani ili na wao waweze kuhudumiwa na hospitali hii na kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa kitovu cha utalii tiba (Medical Tourism) katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Nae, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Dkt. Samia kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya vifaa, vifaa tiba na rasilimali watu katika Sekta ya Afya, huku akimhakikishia mgeni rasmi kuendelea kuhamasisha huduma zinatolewa zinakuwa bora na kusimamia suala la huduma nzuri kwa mteja, lugha nzuri na weledi na miiko ya kitaaluma kwa watoa huduma.
Amesema, Wizara imedhamiria, ifikapo 2025 Hospitali ya Benjamin Mkapa iwe Hospitali ya pili ya Taifa, hij inatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanyika na Serikali, huku huduma za hospitali hizo zikiendelea kusimiwa vizuri na uongozi wa Hospitali hiyo pamoja na watumishi wake.
Pia, amesema, Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa jengo maalumu la kituo cha huduma za uchunguzi na matibabu ya Saratani na tiba mionzi ambalo limefikia asilimia 26, huku likitarajia kuhudumia wagonjwa wote wa kanda ya kati na mikoa ya jirani.
