Kupitia Mkutano na Wanahabari leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mohamed Nasreddine Nabi, ameeleza matamanio juu ya kupata ushindi katika mchezo wa kesho dhidi ya Dodoma Jiji, ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Nabi anasema anaelewa ugumu wa mchezo huo, lakini amewahasa wachezaji wa timu hiyo kupambana, ili kupata alama tatu zitakaowafanya kuwa mabingwa kwa mara ya pili mfululizo.
“Mchezo wa kesho ni muhimu kwetu, tunataka kushinda ili kumalizana na hesabu za ligi, tukicheza vizuri tutatengeneza morali kuelekea kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Marumo Gallants,” alisema Nabi.
Kwa upande wake mshambualiji wa Yanga, Fiston Mayele anasema wanataka kumaliza kazi siku ya kesho.
“Sisi sio mashabiki furaha ya juzi imeshapita, kesho tuna jukumu la kuzitafuta alama tatu, ili tuwe mabingwa,” amesema Mayele.
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope, amesema hawatokubali Yanga kutangaza ubingwa kupitia timu yake.
“Tutatumia mapungufu yao tuliyoyaona ili na sisi tuweze kupata matokeo, mchezo huu umekuja wakati ambao tuna uhitaji mkubwa na alama tatu,” amesema Liogope.
Ikiwa Yanga watashinda mchezo huo watajihakikishia ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara kwa mara ya 29.