Mbunge wa Mbulu Mkoani Manyara, Flatey Massay amesema hatapiga tena sarakasi bungeni kudai kujengewa barabara kwani Serikali imeshaanza ujenzi wa barabara ya lami jimboni kwake.
Amesema anaishukuru serikali ya awamu ya sita kuanza ujenzi wa barabara hiyo ina umuhimu mkubwa tangu Mbulu ianzishwe mwaka 1905.
“Jumatatu ijayo mnatarajiwa kusoma bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi jijini Dodoma bungeni kwa mwaka 2023/2024 hivyo sitapiga sarakasi zaidi ya kusema asanteni,” amesema Massay.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanrodos), Mhandisi Rogatus Mativila amesema kipande cha kilomita 25 kutoka Labbay hadi Haydom kitagharimu Tsh billioni 42.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere amesema Manyara ina changamoto za barabara za lami kuunganisha wilaya zake.
Massay akiwa bungeni Mei 23 mwaka 2022 alipiga sarakasi akidai kuwa barabara hiyo haijengwi ili hali kila mwaka anaisemea na haitengewi fedha za ujenzi.