Imekuwa ni kawaida kufikiria kuhusu kupata mafanikio kupitia fursa mbalimbali za kibiashara lakini watu wengi hujawa na maswali kuwa ni aina zipi za biashara wanaweza kuanzisha angali bado wana kipato au mtaji mdogo. Ukiwa katika nafasi ya kutaka kuwa mjasiriamali nafsi ya uthubutu inahitajika zaidi katika kutafuta wazo la kipekee au kuongezea katika wazo la biashara iliyopo ili kufikia malengo unayoyataka, haijalishi una kipato cha chini, kati au juu.
Kuna Biashara nyingi ambazo unaweza kuzifanya kupitia kipato au mtaji mdogo na kutimiza malengo makubwa ulio nayo katika maisha, inaweza kukugharimu kuanzia uwano wa 1 Tsh. 10,000 -100,000 au gharama ya juu inaweza isizidi Tsh. 250,0000 kama uatanunua mahitaji mengi zaidi.
Yafuatayo ni baadhi ya mawazo ya kibiashara ambayo unaweza ukachagua moja wapo na kulifanyia kazi ili ufanikishe malengo yako;
1. KUUZA JUISI NA ICECREAM
Kujifunza kutengeneza juisi au ice-cream haitakuchukuwa muda sana kuwa mzoefu. Ili ufanikiwe katika biashara hii, cha muhimu ni kujitofautisha. Muhimu zaidi unapofanya biashara ya kutengeneza juisi au icecream, ni kuweka mazingira yako safi na salama kwa wateja wako. Uzuri wa biashara hii ni kuwa mtaji wake ni mdogo sana.
Elfu kumi tu inatosha kuanzia na wapo waliofanya hivyo na wamekuza biashara zao kama vile Mak Juice au Zanana Juice Box.
2. KUPIKA KWA ODA
Kama wewe mwenyewe ni unajiujua ni mpishi mzuri au una mtu anayejua kupika, basi jitangaze kama unapokea oda za mapishi fulani. Tuchukulie unaweza kupika makande au wali nyama vizuri.
3. KUPIGA PICHA
Tangu kuja kwa mitandao ya jamii kama vile Instagram, watumiaji wa mitandao hiyo hutaka picha nzuri. Hapo ndipo unapojitokeza wewe na kuwapa huduma yako ya kupiga picha. Upigaji wa picha ni fani kama fani yengine, ili ujitofautishe pendelea kujifunza kwa wanaojua au tumia YouTube kujifunza.
Vifaa vya upigaji picha vina gharama ila sio lazima viwe vyako, muhimu ni kuwa na ujuzi. Vifaa unaweza kumuazima rafiki yako au kukodi.
Unachoweza kufanya ni kwenda maofisi ya karibu yako na kuwaambia kwamba wakutafute wanapohitaji hicho chakula wakati wa mchana na wewe utawaletea. Usisahau kuacha mawasiliano yako ili waweze kukutafuta. Wengi wao watapenda hiyo huduma kwasababu hawatohitaji kutoka tena kufata chakula.
4. KOCHA WA MAZOEZI (TRAINER)
Kama ilivyo ada kuwa hakuna kitu chenye thamani kubwa kwenye maisha kama afya bora. Watu wengi wamegundua sikuhizi juu ya umuhimu wa kula vizuri na kufanya mazoezi ili kulinda afya zao. Hivyo, baada ya kupata ujuzi nzuri kuhusu mazoezi, anza kawafundisha watu. Utalipwa kwa ujuzi na muda wako.
5. KUPANGA SHEREHE/MATUKIO (EVENT PLANNING)
Kuanzia maharusi, kitchen party, send – off na sherehe nyenginezo nisizozifahamu. Zote hizi ni fursa ambapo unaenda kusaidia watu kuandaa sherehe zao mwanzo mpaka mwisho. Wewe ndio unaumiza kichwa kutafuta watu na huduma mbalimbali kama vile wapambaji, ma DJ, au kuwatafutia gari ya kukodi, kuwapikia chakula na megine mengi. Unachohitaji kuweza kufanya biashara hii ni uwe unawajua watu husika wanaotakiwa kwenye sherehe hizo.
Mfano, ujue wapambaji wa ukumbi, wapishi wa maharusi, maDJ ili uweze kuwapa kazi hizo. Utalipwa kwa kufanya kazi hiyo.
6. UREMBO (MAKEUP, KUSUKA & KUCHA)
Urembo ni gharama. Wanadada wanataka kupendeza wanapokwenda safari zao kama ni kazini ama shughulini. Uzuri ni kwamba hii ni biashara ya kila siku unayoweza kufanya. Baada ya kufanya utafiti wangu, nimebaini kwamba kufanya makeup, kutengeneza kucha na ususi wa nywele zinalipa vizuri tu. Kuna watu wengi tu wanaendesha maisha yao kupitia biashara hizo. Kwanini wewe ushindwe? Na kama sio mtaalamu, hakuna tatizo.
Chukua muda wako na kujifunza, ndani ya muda utaweza.
7. KILIMO CHA MBOGAMBOGA
Kilimo ni sehemu kubwa ya maisha ya watanzania na wale wa nchi nyingi za Afrika. Kila siku zikienda, kilimo huzidi kuwa ni biashara ya matajiri kwasababu shamba lina gharama kubwa. Licha ya hivyo, bado kuna fursa ya kutengeneza kipato kupitia kilimo cha mbogamboga hata kama una mtaji mdogo.
Anza na sehemu ndogo tu unayoweza kupata hata kama ni nyumbani.
8. UFUGAJI WA NDEGE (KUKU, BATA, N.K)
Hii ni biashara ambayo ina faida kubwa lakini pia ina changamoto zake kama vile kuku wako kufa. Vifo vya mifugo huwaumiza sana wafugaji na mara nyingi husababishwa na mifugo hiyo kula uchafu. Hivyo, unapoingia kwenye ufugaji jitahidi uwe na mazingira safi na salama kwa mifugo yako. Usafi wa mara kwa mara hasa hasa kwenye malisho yao utahitajika.
Kwa vile mtaji ni mdogo, unaweza kuanza na kuku wa kienyeji, bata au hata njiwa. Japo kuwa wanachukuwa muda ila kuwa mvumilivu, faida utaiona.
9. KUTENGENEZA TOVUTI (WEBSITES)
Tuko katika ulimwengu wa habari na teknolojia, hivyo kampuni ama biashara ambayo hawako mtandaoni wanakosa wateja. Ichangamkie fursa hiyo kwa kujifunza kutengeneza websites kupitia YouTube. Kisha, tafuta biashara/ makampuni ambayo hawana tovuti na uwaelezee umuhimu wa kuwa na tovuti. Mwisho, waambie kuwa wewe unatoa huduma hiyo.
Kwa kuanza, wateja wako wa mwanzo unaweza kuwafanyia kwa bei ya punguzo halafu mbeleni ukapandisha. Njia hii itakusaidia kupata mabalozi watakao kupatia wateja wengine.
10. KUUZA VOCHA ZA SIMU
Vocha! Tunanunua karibia kila siku. Faida yake sio kubwa kihivyo ila ukizingatia kazi ni ndogo ya kufanya kwasababu vocha zinajiuza wenyewe. Vocha sio kitu cha kutumia nguvu kuuza muhimu watu wajue tu kama unauza vocha. Unaweza kuona vocha zinauzwa kila sehemu kwamba utakosa wateja … lakini sio kweli, kuna sehemu nyingi tu ambazo hakuna muuza vocha karibu.
Anza kuwauzia watu unaoishi nao, majirani au hata wanafunzi wa chuo.