Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa kadi zake mpya za kielekroniki za zitaweza kutumika kama kadi ya kufanyia miamala ya kifedha (ATM).
Katibu wa Taasisi ya CCM, Issa Haji Gavi amethibitisha hilo kwa kusema kuwa kadi za uanachama za chama hicho zitaweza kutumika kwa huduma nyingine ikiwamo kufanya miamala ya kifedha.
Amesema mbali na miamala ya fedha, kwa wanaotumia huduma za Bima ya Afya wataweza kuitumia kadi hiyo pamoja na wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Aidha akizungumza katika kikao cha balozi shina namba 7, Kijiji cha Ilambilole, Jimbo la Isimani, Gavi ameeleza kuwa huduma hizo ndizo zimepelekea kuchelewa kwa kadi hizo.
“Mabadiliko ya kimfumo ndiyo yamesababisha zichelewe, tulikuwa tunafanya mabadiliko ya kimfumo ili tupate kadi zenye sifa. Kuanzia mwezi wa nane kila mtu atakuwa na kadi,” amesema Gavu.
Amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kuunga mkono chama hicho kwa kuhakikisha inashinda tena chaguzi zote zijazo.
Awali baadhi ya wanachama walilalamika kukosa kazi za kielektroniki licha ya kujisajili.
“Kati ya wanachama wote wa shina letu 42, ni nane tu ndio wanazo kadi,” amesema Helena Kiliwa, ambaye ni mkazi wa Kihorogota.
Awali, Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema alisema wanaendelea kusimamia na kuhakikisha yale yaliyoahidiwa yanatekelezwa.