Mlinda lango nambari moja Simba SC, Aishi Manula atakuwa nje ya Uwanja kwa muda wa miezi minne baada ya kufanyiwa upasuaji wa nyama za paja nchini Afrika Kusini.
Manula amefanyiwa upasuaji huo jumanne Mei 30 baada ya kupata majeraha katika mchezo wa Robo Fainali ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Ihefu uliochezwaAprili 7, mwaka huu.
Jana jioni Manula ameruhusiwa kutoka hospitali na leo mchana ataanza safari ya kurejea nyumbani ambapo atafika Jumapili.
Daktari wa timu Edwin Kagabo ambaye yupo naye chini Afrika Kusini amesema baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali, Manula ataingia kwenye sehemu ya pili ya matibabu yake.
Dk. Kagabo amesema sehemu ya pili ya matibabu itakuwa kufanya kliniki ya mazoezi ya viungo (Physiotherapy) kwa utaratibu maalum ili apone vizuri.
“Manula ameruhusiwa kutoka hospitali leo na kesho tutaanza safari ya kurudi nyumbani. Anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa miezi minne ili kupona kabisa.”
“Katika kipindi hiki Manula atapaswa kuhudhuria kliniki ya mazoezi ili kumsaidia jeraha lake lipone vizuri,” amesema Dk. Kagabo (Taarifa kamili kutoka Simba SC App)
“Matibabu ya Upasuaji kwa Mlinda Mlango wetu @28_manula yamekamilika, Al hamdullilah Taarifa kamili juu ya maendeleo yake na muda atakaokaa nje ya dimba ipo kwenye Simba App Get well soon nyanda, Tutakumic” amethibitisha kupitia Twitter Ahmed Ally- Meneja Habari na Mawasiliano Simba SC