Dar es Salaam, Jana Juni 12, 2023 Shirika la ndege la Air France kutoka nchini Ufaransa wamezindua safari yake ya kwanza ya ndege kutoka Paris Charles de Gaulle (CDG) hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo jijini hapa.
Kuanzishwa kwa safari hii mpya, Air France inaonyesha imani na Tanzania kama kivutio cha safari za biashara pamoja na zile safari za kifahari. Huku muda wa kutua nchini ikiwa ni saa 4:20 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, safari hiyo inatajwa kuwa ni mwendelezo wa huduma za shirika hilo kutoka Paris hadi Zanzibar.
Huduma hizo za usafiri zitakua zikitolewa mara tatu kwa wiki ambapo itakua ni siku za Jumatatu, Jumatano na Jumamosi, na zitakuwa zikitolewa na ndege aina ya Boeing 787-9, ikitajwa kuwa ndege bora inayoendeshwa na Shirika la ndege Air France, ikifanya safari zake katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.
Akizungumzia kuanzishwa kwa safari hiyo mpya, Meneja Mkuu wa Air France-KLM kwa Afrika Mashariki na Kusini, Nigeria, na Ghana Marius van der Ham, alisema,
“Huu ni wakati mzuri wa kujivunia kwa Air France tunapoendelea kuongeza huduma zetu barani Afrika. Tuna imani kuwa kuanzishwa kwa safari hii mpya italeta manufaa makubwa kwa Tanzania na Ufaransa, na kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni na kiuchumi kati ya nchi zetu mbili.” Alisema Van der Ham.
Hata hivyo amesema kuongezwa kwa huduma hii ya usafiri wa ndege, inatazamiwa kuwapa wasafiri chaguo zaidi na kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii nchini Tanzania.
Ratiba hii mpya itawawezesha abiria wanaopanda AF876 kuondoka Charles de Gaulle saa 4:30 asubuhi (AM) na kuwasili Dar es Salaam saa 4:20 usiku (PM) wakati huo ndege hiyo ikitokea katika kituo cha Zanzibar saa 2:15 usiku. Baada ya kuwasili nchini kwa safari za kurudi ndege itakua inaondoka Dar es Salaam saa 5:50 usiku huku ikitarajiwa kutua Charles de Gaulle saa 1:55 asubuhi.
Abiria waliokuwa katika uzinduzi wa safari mpya za ndege hiyo walikaribishwa vyema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Huku wakipokelewa na Waziri wa Uchukuzi, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa,Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Nabil Hajlaoui na wawakilishi wengine kutoka serikalini na sekta ya utalii.
Katika salamu zake za ukaribisho, Meneja wa Air France – KLM nchini Tanzania Alexander van de Wint, ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya kibiashara. “Tunafuraha kuweza kuwaunganisha wateja wengi zaidi kutoka Tanzania, Dar es Salaam hadi Paris na kwingineko kwa zaidi ya vituo 200 duniani kote, na kutoa fursa zaidi kwa wateja kupata uzoefu wa maeneo mengine barani Ulaya na kwingineko duniani.”