å
Dar es Salaam, 15 Juni 2023: Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji ya Umoja wa Mataifa (UNCDF), mtekelezaji mkuu na meneja wa mfuko wenye thamani ya Euro milioni 17 wa programu ya CookFund, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), umezindua kampeni ya uhamasishaji iitwayo Anzia Jikoni – change for a cleaner future starts in the kitchen.
Uzinduzi huo ulifanyika katika wa warsha ya vyombo vya habari iliyoandaliwa na Shirika hilo la Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kubadilishana ujuzi juu ya jinsi matumizi ya teknolojia safi ya kupikia, yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kutatua changamoto za afya, mazingira na kijamii. Pia warsha hiyo iliangazia hitaji la umma, washirika wa maendeleo na sekta binafsi katika kushirikiana kuhakikisha kuna uendelevu wa matumizi ya teknolojia safi za kupikia.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Senior Finance Specialist and CookFund Programme Manager, UNCDF Tanzania, Bw. Imanuel Muro, alisema, “Ufadhili wa EU unasaidia, na kuongeza utaalam wetu katika uwekezaji wa kifedha ili kuleta maendeleo endelevu, na pia kuchochea uwezo wa makampuni katika kuvumbua teknolojia safi za kupikia. Pia kupitia kampeni yetu ya Anzia Jikoni, tutaweza kuonyesha umuhimu na faida za kutumia teknolojia hizi.”
Zaidi ya hayo, data kuhusu nishati za kupikia nchini zinaonyesha asilimia 85 ya watu wanatumia biomasi, na hivyo ndio maana programu ya CookFund inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), inalenga kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kuanzia jikoni. Bw. Imanuel Muro aliongeza, “Kama waandishi wa habari, mna jukumu muhimu katika kuwasilisha umuhimu wa mabadiliko katika teknolojia za kupika ili kuchangia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu”.
Programu ya CookFund yenye thamani ya Euro milioni 17 Iko chini ya ‘Mpango wa kutumia nishati safi ya Safi ya Kupika nchini Tanzania,’ na Mfuko wa 11 wa Maendeleo ya Ulaya (EDF), na unaunga mkono mipango ya serikali ya kuongeza upatikanaji wa nishati safi. Mpango huo unalenga matumizi ya 80% ya ufumbuzi wa kupikia safi ifikapo 2033.