Dar es Salaam Tanzania, Tarehe 19 Juni 2023 Azam Media LTD [AML] na Studio za PowerBrush [PBS] , zinapenda kuuarifu umma wa watanzania wote kuwa mipango yote muhimu imekamilika tayari kwa uzinduzi ya kwa filamu yetu ya Ugunduzi wa kisayansi ya EONII.
Onyesho hilo la kwanza la uzinduzi wa kihistoria utafanyika Ijumaa, Juni 23, 2023, kwenye Ukumbi Century Sinemax Mlimani City Dar es Salaam, ambapo tunategemea kuwa na onyesho maalum kwa wageni waalikwa wakipata fursa ya kushuhudia Filamu hii.
Tutumie fursa hii kwa niaba ya Azam Media LTD na PowerBrush Studios kutambua mchango mkubwa wa serikali yetu katika kusimamia michezo na sanaa nchini na kuweka mipango endelevu ambayo tunashuhudia matunda yake kupitia mageuzi haya kwenye tasnia ya Filamu Nchini.
Bodi ya Filamu wamekuwa mhimili mkubwa katika kutoa hamasa, kuratibu njia sahihi za kuisukuma sanaa yetu ya Filamu na Kipekee kabisa tunasema Ahsante sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka chachu inayoipeleka sasa sanaa yetu ya filamu kimataifa.
Kufuatia Hamasa hizi na sera na kanuni madhubuti; timu yetu ya uzalizashaji pamoja na PowerBrush Studios wamewekeza katika ubunifu na umakini mkubwa kuandaa filamu ya EONII ambayo inasukuma mipaka ya kuwaza na kusimulia hadithi. Juhudi hizi za kipekee ni uthibitisho wa kukua kwa vipaji na matamanio ndani ya tasnia ya filamu Tanzania.
Ni matarajio yetu viongozi na waalikwa wengine watakuwa mabalozi wazuri baada ya Onyesho la awali la Premier siku ya Ijumaa tarehe 23 Juni 2023 pale Mlimani City; Mbali na onyesho kuu la Dar es Salaam, EONII itaonyeshwa katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Tanga na Mwanza kwa upande wa Tanzania Bara, huku Zanzibar ikiwa kituo muhimu ambako tunategemea kutumia mafuriko ya watalii kwa sasa kufuatia hamasa ya Royal Tour kuwapa ladha hii ili nao warejeshe taarifa hizi za mageuzi katika filamu nchini na kuongeza thamani katika safari zao za Kitalii; kwamba ukipata fursa ya kuja Tanzania hutoshia kwenye vivutio vya utalii pekee bali burudani ya aina yake kutoka kiwanda cha filamu chenye vionjo vya kipekee vyenye hadhi ya kimataifa na kushajihisha vema utamaduni wa mtanzania.
Tunatambua kiu na shauku ya kufahamu tarehe hizi na maeneo kutakapotazamwa Filamu hii ni kiu ya kila mtanzania; lengo letu ni kuisogeza karibu na katika kumbi rafiki kwa watu wa rika zote na hivyo maelezo zaidi na matangazo juu ya wapi, saa ngapi na lini yatatolewa wakati wa usiku wa onyesho la kwanza pale Mlimani City tarehe 23 Juni 2023.
Lengo letu ni kuhakikisha Maonyesho haya ya katika majiji yetu yanauleta ulimwengu wa kuvutia wa filamu za kisanyansi na kuibua ubunifu na shauku ya kutazama filamu zote kupitia filamu yetu ya EONII.
Mafanikio ya filamu ya EONII si uthibitisho tu wa maono ya ubunifu wa timu na ari yake bali pia ni fursa kwa wapenzi wa Sanaa na Burudani na wadau wengine katika nyanja hii kusaidia filamu zetu za Tanzania kustawi maradufu. Na hapa kipekee niwaombe wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, viwanda, wafanyabiashara na wadau katika sekta nyingine za uzalishaji kuwa sehemu ya filamu hizi kwa kuwezesha udhamini na ufadhili wa moja kwa moja kwa wasanii wetu.
Nimalizie kwa kusema AML na PBS inawaalika waheshimiwa wanahabari, wataalamu wa tasnia ya filamu, wageni mashuhuri, na wapenzi wa filamu kujumuika nao kwenye Jumba la Sinema la Mlimani City siku ya Ijumaa, Juni 23, 2023, ili kushuhudia uzinduaji wa filamu hii muhimu ya Science Fiction (sci-fi) EONII.
Tukio hili tunawaahidi litaweka alama na halitosahaulika haraka katika safari hii ya mapinduzi makubwa katika kiwanda cha Filamu za Tanzania. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania; Mungu wabariki wasanii wa Filamu na na Kazi zao.