Ikiwa ni sehemu ya kusaidia walaji kutoa maoni yao juu ya ubora wa bidhaa na huduma wanazozipata sokoni, tuzo za Consumer Choice Awards Africa (CCAA) mwaka huu zinatarajia kushindanisha makampuni mbali mbali katika aina zaidi ya 70 za tuzo.
Akizungumza katika uzinduzi wa tuzo za mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa CCAA Diana Laizer alisema mashindano ya mwaka huu yatahusisha aina kuu 22 za tuzo pamoja na nyingine ndogo ndogo zaidi ya 70.
Alitaja aina za tuzo zitakazoshindaniwa kuwa ni pamoja na Usafirishaji, Mawasiliano ya simu, Usafiri wa Anga, Huduma za kifedha, Ujenzi, Huduma za Bima, Mafuta na Gesi, Hoteli ,Usalama, Bidhaa zinaotoka haraka, Matukio na Mapambo, Mitindo na Ubunifu, pamoja na Upigaji picha.
“Katika kipindi cha miaka 4 iliyopita, tumeweza kufikia maelfu ya wateja barani Afrika kupitia njia ya mtandao na kukusanya maoni yao juu ya bidhaa na huduma wanazotumia na zaidi ya tuzo 70 zimekuwa zikitolewa kila mwaka. Tunajivunia mafanikio haya”. alisema
Akizungumzia mchakato wa kuwapata washindi, Diana alibainisha kuwa washindi wa tuzo hupatikana kupitia utaratibu wa kupiga kura mtandaoni ambapo walaji wana nafasi ya kupigia kura bidhaa au huduma mbali mbali zinazoshindanishwa kupitia tovuti ya CCAA”.
“Baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa washiriki katika makundi tofauti, timu yetu inafanya kazi ya kupanga makundi hayo kulingana na mapendekezo na vigezo vya tuzo husika. Zoezi hili likikamilika makundi huwekwa mtandaoni na walaji huweza kupiga kura kulingana machaguo yao. Upigaji kura hufanyika kwa siku zisizopungua 25 na mlaji anaweza kupiga kura mara moja tu katika kila aina ya tuzo,” alifafanua
Kwa mujibu wa Diana, baada ya muda wa kupiga kura kumalizika, mfumo huonyesha matokea kulingana na idadi ya kura ambazo bidhaa au huduma imepigiwa.
“Dirisha la kupendekeza aina za tuzo kwa mwaka 2023 limefunguliwa rasmi kuanzia leo tarehe 18 Juni 2023 na litaendelea hadi tarehe 9 Julai 2023. Zoezi la upigaji kura litatangazwa baadaye mwaka huu kwa hivyo tunayahimiza makampuni na chapa kushiriki na kushirikisha wateja wao,” aliongeza.
Mkurugenzi huyo aliyapongeza makampuni ambayo yamekuwa yakishiriki na kuwahamasisha wateja wao kuyapigia kura.
Mwanzilishi wa tuzo za Consumer Choice Awards Africa(CCAA) Diana Laizer, akiongea wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo kwa mwaka 2023. Hafla ya uzinduzi ilifanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau pamoja na wadhamini wa tuzo hizo.
Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Latifa Khamis akiongea kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji , Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaju wakati wa uzinduzi wa tuzo za Consumer Choice Awards Africa(CCAA) jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi mtendaji wa Koncept Group Krantz Mwantepele (kulia) akiteta jambo na mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Latifa Khamis kushoto pamoja na mwanzislishi wa tuzo za Consumer Choice Awards Africa(CCAA) Diana Laizer muda mfupi baada ya uzinduzi wa tuzo za mwaka 2023.
Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi wa tuzo za Consumer Choice Awards Africa (CCAA) wakifuatilia matukio wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo uliofanyika jijini Dar es Salaam.