Kampuni ya Ndege Air Tanzania (ATCL) Jana imeanza rasmi safari yake ya kwanza ya kusafirisha mizigo kwa kutumia ndege yake ya mizigo ya Air Tanzania Cargo aina ya Boeing 767-300F iliyowasili nchini mapema mwezi Juni 2023 ambapo mzigo wa leo unasafirishwa moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Dubai kwa muda wa Masaa tano tu.
Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni hiyo Patrick Ndekena amesema ratiba ya safari za Dubai itakuwa mara mbili kwa wiki ambapo jukumu la ATCL kwa ndege hii ni kuhakikisha bidhaa za Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi zinafika kwa wakati na zikiwa na ubora wake kwenye Nchi mbalimbali kwa kadri ya mahitaji.
Kuhusu uwezo wa ndege hiyo, amesema Boeing 767-300F ni ndege ya kisasa yenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 850 kwa saa na kukaa angani kwa zaidi ya saa 10 bila kutua.
Kwa upande wake Wakala wa usafirishaji mizigo George Magoti amesema uwepo wa ndege hii ni Mkombozi kwa Wafanyabiashara nchini kwani itawasaidia kupunguza gharama za usafirishaji ambapo amesema kutokana na ukubwa wa mizigo hii, isingewezekana kusafirishwa kwa ndege ya abiria hivyo wangelezimika kukodi ndege ya mizigo kutoka nje ya Tanzania ili kuweza kupakia mizigo mikubwa ya aina hii.