Wanyonyi alisema alinuia kumwadhibu Mandonga ambaye awali alimshinda kwa kipigo cha kiufundi (Technical) katika pambano lisilo la ubingwa la uzani wa super middle weight lililoandaliwa katika Ukumbi wa Kenyatta International Conventional Center (KICC) jijini Nairobi Januari mwaka huu.
Kufuatia ushindi wake wa Jumamosi, bondia huyo wa Kenya alisema angeweza kumaliza pambano hilo katika raundi za mapema, lakini alijizuia kwa kuwaheshimu mashabiki.
Kulingana naye, alitaka kuwapa mashabiki thamani ya pesa zao kwa kuandaa mechi ya kuburudisha.
“Ingawa nilimwangusha mara mbili, sikutaka kumtoa mchezoni mapema. Nilikuwa na wasiwasi kwamba mashabiki hawangepata thamani ya pesa walizolipa kutazama pambano ikiwa ningemaliza mchezo mapema,” Wanyonyi alisema.
Aliongeza: “Nilikuwa na uhakika kwamba hangeweza kunipiga wakati huu, kwa hiyo nikamwadhibu. Nina hakika hakupata usingizi mzuri.”
Alihusisha ushindi wake na maandalizi ya kutosha aliyojiwekea kabla ya kukutana na Mandonga katika pambano lisilo la ubingwa ambalo lilifanyika Sarit Centre Expo jijini Nairobi wikendi iliyopita.
Wanyonyi aliibuka mshindi kwa pointi baada ya kuwatoa Mandonga katika raundi ya sita na kumi ya pambano hilo lililokuwa likitarajiwa.
Kwa upande wake, Mandonga, ambaye alidhibiti pambano vyema katika raundi tatu za kwanza, alimpongeza Wanyonyi kwa ushindi wake, lakini aliapa kulipiza kisasi kwa bondia huyo wa Kenya katika mechi yao inayofuata.
“Hakuna kitu kibaya kilichotokea, nimepoteza pambano hili, nampongeza, leo ameshinda, kesho nitakuwa mimi,” alisema Mandonga.
Kufuatia ushindi wake wa Jumamosi, rekodi ya Wanyonyi sasa iko (29-15-2), wakati rekodi ya Mandonga iko (6-4-2).