Katika jitihada za kuhakikisha inatengeneza usawa na ujumuishi wa mazingira bora ya ufikiwaji wa huduma zake na wateja wake wote nchini, kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC imezindua dawati la huduma kwa wateja kwa watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika kwenye duka la huduma kwa wateja lililopo makao makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Bw. Philip Besiimire amesema kuwa siku zote kampuni inajitahidi kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma zake kuhakikisha zinawafikia na kuwanufaisha wateja wote bila ya ubaguzi.
“Uzinduzi wa dawati la huduma kwa watu wenye ulemavu ni muendelezo wa uboreshaji wa njia mbalimbali za kutoa huduma jumuishi na kutengeneza mazingira mazuri kwa wateja wetu. Vodacom tumewapatia wateja takribani njia 30 za kujihudumia wenyewe na kutufikia wakiwa wanahitaji huduma yoyote kutoka kwetu. Miongoni mwa huduma hizo ipo huduma ya IVR (Instant Voice Response) ambayo haimuhitaji mteja kuzungumza na mtoa huduma moja kwa moja hivyo kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu. Leo tunayo furaha kuzindua rasmi dawati la huduma mahususi kwa watu wenye ulemavu ambalo tunaamini kuwa litakuwa ni msaada mkubwa kwao kupata huduma sawa na wengine,” alielezea Bw. Besiimire.
Mpaka kufikia hatua ya kuweka dawati la huduma maalamu kwa watu wenye ulemavu, Vodacom imegundua kuwa itakuwa ni rahisi kwa wao kuwa na watoa huduma wenye taaluma na maarifa ambao watakuwa wamejikita katika kuwahudumia.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja alifafanua zaidia kuwa, “ingawa huduma ya IVR ni msaada mkubwa kwa walemavu lakini bado wanakumbana na changamoto ya kuitumia ipasavyo. Kwasababu huduma hii inamtaka mteja kubonyeza kitufe kitakachomuunganisha na huduma anayohitaji. Lakini kwa kuwatambua wateja hawa, kila wapigapo simu au kutembelea dukani kwetu, wataunganishwa au kukutana na wataalamu wa kuwahudumia bila ya changamoto yoyote.”
“Napenda kutoa wito kwa Watanzania na wateja wetu kwa ujumla ambao wanachangamoto yoyote ya ulemavu wasisite kutembelea maduka yetu ya kutolea huduma kwa wasiwasi kwamba watashindwa kuhudumiwa. Vodacom inafanya jitihada za makusudi kutengeneza na kukuza ujumuishi katika Nyanja tofauti za utoaji huduma zake. Na hii inaenda sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha kuwa hatumwachi mtu nyuma kwenye uendeshaji wa shughuli zetu nchini kote,” aliongezea Bw. Besiimire.
Kwa kumalizia akifafanua zaidi kuhusu kukuza ujumuishi, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania alibainisha kuwa, “tunajivunia kuwa mpaka sasa takribani wateja 8,797 wenye ulemavu wamekwisha hudumiwa. Tumeboresha maduka yetu 147 na kuwa na barabara zinazowawezesha walemavu wanaotumia viti vya magurudumu kuingia kwenye maduka yetu ya kutolea huduma kwa urahisi. Pia, tunayo huduma ya lugha za alama katika kwa wateja wenye changamoto ya kusikia inayopatikana kwenye maduka 64 nchini kote. Hii inaenda sambamba na huduma ya lugha za alama kwa picha jongefu (video) kwa wateja ambao wako mbali na maduka yetu. Kuhakikisha huduma hizi zinatolewa kwa weledi mkubwa, watoa huduma wetu takribani 30 wamepatiwa mafunzo ya kutosha. Lengo kubwa ni kuhamasisha jamii nzima pia izingatie ujumuishi wa utoaji wa huduma hivyo tunaendelea na kampeni za kuhamasisha vikundi mbalimbali ikiwemo taasisi za watu wenye changamoto ya kusikia (viziwi)”.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Baraza la Ushauri la Huduma za Mawasiliano la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Bw. Gideon Mandesi amesema kuwa, “jitihada hizi za Vodacom zinazoonyesha utekelezaji wa sheria kuhakikisha makundi ya walemavu kama vile viziwi na wasioona. Maboresho ya huduma hii ni muhimu kwasababu watawezesha si mawasiliano pekee bali hata kujiajiri. Nawapongeza pia kwa kutambulisha simu rafiki na zenye gharama nafuu, muendelee kuboresha zaidi kwasababu uhitaji bado ni mkubwa zaidi. Serikali inaendelea kuweka utaratibu wa sheria na kanuni ili wawekezaji kuendelea kutoa huduma jumuishi. Nawapongeza kwa hili na kuboresha miundombinu yenu ya kutolea huduma na nawaomba kuwasihi wafanyakazi wenu kote nchini kuwahudumia wenye ulemavu kwe weledi. Pia, huduma hii iwe endelevu kwa kuongeza uwekezaji zaidi”.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyochapishwa na taasisi ya SEVA kwa mwaka wa 2022-2023, inaonyesha kuwa asilimia 0.5 ya idadi ya Watanzania wanachangamoto ya kuona au vipofu (ambayo ni sawa na watu 293,392), ukilinganisha na asilimia 0.19 ya idadi ya Wamarekani. Ripoti hii inaendelea zaidi kwa kuelezea kuwa asilimia 1.73 ya idadi ya watu wapo katika hatari ya kiwango cha kati na juu ya kupata upofu (sawa na watu 1,020,266), ukilinganisha na asilimia 2.02 ya idadi ya Wamarekani.
#KonceptTvUpdates