Serikali imesema itaendelea kuboresha na kujenga miundombinu ya vituo vya afya pamoja na kuweka mikakati inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote ili kuimarisha kinga na Tiba ya Maradhi ya Saratani
Hayo yameelezwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Februari 06, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha uwekezaji na wadau wa maendeleo kwa ajili ya uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri wa Matibabu ya Saratani nchini Tanzania.
Kituo ambacho kitakuwa pekee cha umahiri wa matibabu ya Saratani katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Maradhi ya Saratani ni ugonjwa unaoathiri mamilioni ya watu kote ulimwenguni, hivyo kama jamii tunapaswa na sisi kuwekeza katika kinga na tiba ya maradhi haya, tayari Serikali imeanza kuchukua hatua na tunashuhudia hatua katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za afya na mikakati inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa wote” amesema Dkt. Mwinyi.
Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa uwekezaji katika huduma za Saratani nchini unakusudia kujenga matumaini ya maisha kwa watu na familia ambazo zimekubwa na changamoto hiyo.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mtu anaekutana na changamoto ya Saratani anapata huduma kamili na matibabu stahiki, Maono ya Mhe. Rais Dkt Samia yanalenga mbali na kuzingatia maendeleo endelevu ikiwemo matumizi ya nishati mbadala kukuza uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali zetu za asili, malengo haya yanaonesha dhamira ya dhati ya kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadae, juhudi hizi ni sehemu ya Mkakati wa kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani” amesema Dkt. Mwinyi.
Aidha Rais. Dkt. Mwinyi akatumia fursa hiyo kuhimiza juu ya umuhimu wa ushirikiano utakaosaidia kutimiza malengo ya nchi na kuhakikisha upatikanaji wa matibabu bora kwa wagonjwa wa Saratani.
“Kwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, watafiti na wataalam wa tiba tunaweza kubadilisha kabisa taswira ya huduma za saratani, tuwe na dhamira ya dhati ya kufanya kazi bila kuchoka katika kukabiliana na ugonjwa wa Saratani ili kuleta matumaini kwa wale watakaopata changamoto hio ya kiafya” amesema Dkt. Mwinyi
#KoncepTvUpdates