MAELFU ya wananchi wa wilaya ya Temeke, hususani wakazi wa Mbagala na vitongoji vyake, wamefurika vilivyo katika Tamasha la Kuhamasisha Ufunguaji wa Akaunti Nafuu Isiyo na Makato ya Mwezi inayotolewa na Benki ya NMB ‘NMB Pesa Day.’Tamasha hilo limefanyika mwishoni mwa wiki kwenye Viwanja vya Mbagala Zakhiem, likienda sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde itakayodumu kwa miezi mitatu, ambako mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda.
Katika tamasha hilo lililotanguliwa na mbio za taratibu ‘jogging’ na burudani za muziki kutoka kwa wasanii kama Miso Misondo na Wazee wa Makoti, Mr Blue, Dulla Makabila na wengineo, DC Mapunda aliipongeza NMB kwa ubunifu katika kusambaza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa wananchi.
DC Mapunda alisema kwamba NMB Pesa inaenda kuwa chachu ya maisha bora kwa wana Temeke na Watanzania kwa ujumla, ambako licha ya ‘jogging,’ wahudhuriaji walipewa elimu na huduma za kifedha, mashindano ya vipaji vya muziki, ambako zawadi mbalimbali zilitolewa na DC huyo kwa washindi.
“Tupo hapa kwa ajili ya NMB, ambayo inafanya kitu kikubwa sana leo kwa ustawi wa maisha yetu. Kwa kutuletea NMB Pesa, ambayo kwa shilingi 1000 tu, unafungua akaunti hata ukiwa na simu ya kitochi, akaunti ambayo itakuwezesha kupata huduma zote za kifedha, ikiwemo mikopo, kutuma, kupokea, kutoa fedha na kulipia bili mbalimbali.
“Sasa, mimi niwaombe kitu kimoja Wana Mbagala, sisi tupo wengi sana na ‘buku buku’ zipo nyingi sana miongoni mwenu, changamkieni fursa kwa kufungua akaunti za NMB Pesa ili mujiwekee akiba, lakini mpate kunufaika na huduma za kifedha za benki hii.
“Hapa kuna droo nyingi zinaendelea kwa wote wanaofungua akaunti sasa, ambapo watajishindia pesa taslimu, majiko na mitungi ya gesi, baiskeli za tairi tatu ‘guta,’ na zawadi kubwa zaidi ya bodaboda ambayo nitaikabidhi mwishoni mwa tamasha hili. Kwa hiyo changamkieni fursa,” alibainisha.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, aliwahakikishia Wana Mbagala na Watanzania kwa ujumla, kwamba NMB imewaletea fursa inayoenda kubadili maisha yao, kupitia NMB Pesa Akaunti, ambayo ni ya kidigitali unayofunguliwa kwa Shilingi 1,000 tu, ikiwafikia ikiwa na fursa nyingi.
“Fursa ya kwanza inayokuja na akaunti hii ni kuwa unaingia moja kwa moja kwenye Huduma Jumuishi za Kifedha kupitia NMB, watoa huduma wametapakaa kote kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa sehemu ya huduma hii inayokuja chini ya kaulimbiu ya ‘Haachwi Mtu.’
“Kupitia NMB Pesa, utakuwa umeingia moja kwa moja katika huduma ya NMB Mkononi, inayokupa wigo mpana wa kujihudumia na kuhudumiwa kibenki bila kuja matawini ama katika ofisi za benki yetu ambako utafanya miamala na malipo na manunuzi kidigitali.
“Pia, rekodi zako kipesa kupitia NMB Pesa Akaunti, zitakuongezea fursa, kwani kubwa kuliko yote utaweza kukopa hadi shilingi 500,000 kupitia Mshiko Fasta, huduma ya mikopo isiyohitaji dhamana yoyote wala kujaza fomu. Hapo vipi, haujabadilisha maisha yako?
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, hii kampeni tunayoianza leo, ni kampeni ya Weka Akiba na Ushinde, kwahiyo pamoja kufungua akaunti ya NMB Pesa, lakini pia tunazindua Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde, yaani unaweka 50,000 na unajishindia zawadi mbalimbali,” alisisitiza.
Bi. Zaipuna alibainisha kwamba, kila wiki kutakuwa na droo zitakazozalisha washindi 10 wa watakaojishindia Sh. 500,000 kila mmoja, washindi watano wa kila mwezi watazoa Sh. Mil. 1 na katika droo ya fainali, mshindi atajinyakulia Sh. Mil. 10, washindi nane wa Sh. Mil. 3, mashine ya kufulia, tv, friji, bodaboda tano pikipiki nane za mizigo
“Kwa mantiki hiyo, tunawakaribisha Watanzania wote wajiwekee akiba, lakini pia wabadilishe maisha na kuboresha biashara zao kupitia akiba na zawadi watakazoshinda,” alisema Bi Zaipuna alipozungumza na maelfu ya waliohudhuria tamasha hilo, lililofungwa kwa Agnes Maujundu kujinyakulia bodaboda ya Sky Mark.