Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeamua kwa dhati kuendeleza vyanzo vya umeme wa Jotoardhi ili kuhakikisha nchi inazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya wananchi wake.
Amesema chanzo hicho cha umeme kitaongeza nguvu katika vyanzo vilivyopo vya Maji na Gesi Asilia. Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 20 Februari, 2024 mara baada ya kukagua vyanzo vya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka (60MW) na Ngozi (MW 70) mkoani Mbeya akifuatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Juma Homera.
” Miradi hii ya Jotoardhi sasa lazima ianze, tutaanza na megawati 10 hapa Kiejo-Mbaka na Ngozi tutaanza na megawati 30 huku nyingine zikifuata, na hii inajumuisha miradi mingine kama wa Jua wa Kishapu (150 MW) ambao umeanza kutekelezwa, miradi ya umeme wa upepo ukiwemo wa Makambako na mradi wa Malagarasi ambao mkandarasi ameshasaini mkataba tayari kwa kuanza kazi.” Amesema Dkt. Biteko
Amewaelekeza watendaji wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) kufanya kazi zinazoleta matokeo na si stori kwani Serikali inatafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo na wajibu wa watendaji wa Taasisi hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona watanzania wanapata huduma bora katika sekta zote, wanatolewa kwenye umaskini, anataka vitendo na siyo maneno, anataka kuona watu wahudumiwa na kufuatwa walipo, wanasikilizwa shida zao na kutatuliwa.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia anataka utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali iangalie miaka mingi mbele na si muda mfupi hivyo ametoa uhakika kwa wananchi kuwa miradi hiyo ya Jotoardhi itatekelezwa.
Kuhusu changamoto ya umeme, amesema kuwa, imetokana na vyanzo vya umeme nchini kwa muda mrefu kujikita kwenye makundi matatu tu ambayo ni maji (570MW), Mafuta na Gesi Asilia.
Amesema kwa sasa, vyanzo vya umeme vinatokana na Gesi Asilia na Maji ambavyo bado havitoshelezi mahitaji kutokana na kuzidi kukua kwa maendeleo, idadi ya watu kuzidi kuongezeka, miji kukua na umeme sasa kuwa ni hitaji muhimu na si anasa.
Amesema pamoja na kutegemea megawati 235 kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) na megawati 27 kutoka Rusumo, maboresho ya mitambo mingine ya umeme yanaendelea katika vituo mbalimbali.
Aidha, amesena kuwa, Serikali imeshaamua kutekeleza vyanzo vingine vya umeme ikiwemo vya Jotoardhi, Jua na Upepo kwani vipo na kinachohitajika ni kuvipa nguvu, Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amepongeza viongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo pamoja na ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa Serikali na Wabunge wa Mkoa huo.
Awali, Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba, amesema kampuni hiyo ina miradi mitano ya kipaumbele nchini ambayo ni Kiejo-Mbaka, Ngozi, Songwe, Ruhoi na Natron.
Ameeleza kuwa, kwa Mkoa wa Mbeya miradi ya kipaumbele ni Ngozi na Kiejo-Mbaka ambapo mradi wa Ngozi unatarajiwa kuzalisha megawati 70 na Kiejo-Mbaka unatarajiwa kuzalisha megawati 60.
Katika mradi wa Ngozi, amesema kuwa, utatekelezwa kwa awamu huku awamu ya kwanza ikitarajiwa kuzalisha megawati 30 na fedha zimeshapatikana ili kuhakiki rasilimali ya Jotoardhi kwenye eneo hilo.
Ameongeza kuwa, mradi huo wa awali utakaozalisha megawati 30 utagharimu Dola za Marekani milioni 144 sawa na shilingi bilioni 369.
Kuhusu mradi wa Kiejo-Mbaka, amesema kuwa, unatarajiwa kuzalisha megawati 60 ambapo zitaanza kuzalishwa megawati kumi (10) ambazo utekelezaji wake utagharimu Dola za Marekani milioni 75.64 sawa na shilingi Bilioni 175.88.
Cc:Wizara ya Nishati