Kazi iliyotukuka ya kutangaza Utalii wa Nchi yetu iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Tanzania “The Royal Tour” inazidi kudhihirisha matokeo chanya katika Hifadhi zetu Nchini hususan Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara ambayo inazidi kupata idadi kubwa ya watalii kutoka Mataifa mbalimbali Duniani Kila uchwao.
Kwa mara nyingine Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Februari 24, 2024 imepokea Kundi la sita la watalii wa kigeni wapatao 146 waliotoka ughaibuni kwa ajili ya kutembelea na kutalii ndani ya Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyopo wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.
Imetajwa kuwa watalii hao wametoka katika Nchi za Australia, Austria, Belgium, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, Poland, Urusi na Hispania huku wengine wakitokea Nchi za Switzerland, Uingereza na Marekani wakisafirishwa na Meli iitwayo “Le Bougainville”.
Watalii hao wameeleza kufurahishwa na upekee wa historia ya Magofu ya Kale, ustaarabu na utamaduni wa wakazi wanaoishi katika Hifadhi hiyo huku wakipongeza jitihada za dhati za kuboresha miundombinu ya utalii zilizofanywa na Serikali kupitia TAWA Hifadhini humo.
“Imekuwa ni safari nzuri kwetu kwasababu tumepata fursa ya kipekee kujifunza historia ya Nchi hii nzuri ikiwa ni pamoja na kukutana na watu wa tamaduni mbalimbali kuona namna wanavyoimba na kucheza, nimependa sana hakika nimependa” Dominick Alexandre mtalii kutoka Ufaransa
TAWA inaendelea kupokea wageni mbalimbali kutoka Kila Kona ya Dunia kupitia Hifadhi hiyo na Hifadhi nyingine zilizo chini ya usimamizi wake, ambapo katika kipindi cha Mwezi Februari kuanzia tarehe 03 mpaka tarehe 24 Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara imepokea Meli za watalii zipatazo sita zikiwa na jumla ya watalii 710 na bado inatarajia kupokea Meli nyingine za watalii ambao watatembelea Hifadhi hiyo.