Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha inafanya maboresho kwenye mitambo ya uzalishaji maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu hususani pampu za kusukuma maji ili kuwezesha huduma ya maji iweze kupatikana kwa ufasaha na kwa wananchi wote.
Mhe. Waziri ametoa maagizo hayo wakati alipotembelea na kukagua hali ya uzalishaji na upatikanaji huduma ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kujiridhisha juu ya upatikanaji wa maji ya kutosha kwenye chanzo cha maji Mto Ruvu.
Ameongeza kwa kusema ameridhishwa na hali ya upatikanaji wa maji kutoka Mto Ruvu na kuwa mitambo ya maji Ruvu Juu na Ruvu Chini maji yapo ya kutosha, hivyo kazi kubwa inayohitaji kufanyika ni maboresho ya pampu za kusukuma maji kwenye ili huduma iweze kupatikana.
“Nipende kuwajulisha wananchi kuwa hakuna shida ya maji kwenye vyanzo vya maji Ruvu Chini na Ruvu Juu, kazi inayofanyika ni kuboresha uzalishaji wa maji hususani mitambo ya kusukuma maji pamoja na kuboresha ufuatiliaji wa maji kwa wananchi,” ameeleza Mhe. Waziri.
Wizara ya Maji itaendelea kuwa kipaumbele katika kufuatilia na kuhakikisha huduma inaimarika kwenye maeneo yote Dar es Salaam na Pwani.
Amewasihi wananchi kulinda vyanzo vya maji vilivyopo ili kuokoa gharama kubwa inayotumika katika kusafisha na kutibu maji kwenye mitambo ya kuzalisha maji.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Adam Ngalawa amesema kuwa viongozi wamejionea kazi inayofanyika na wameridhika kwa kuona fedha zinazotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan zimetumika kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
“Tumeona pia uwepo wa maji kwenye vyanzo vya maji na kazi kubwa inayofanywa na DAWASA kuboresha miundombinu ya uzalishaji maji ili huduma ifike kwa wananchi ipasavyo,” amesema Mhe. Ngalawa.
Naye Meya wa Kinondoni Mhe. Sengoro Mnyonge ameipongeza DAWASA kwa kazi kubwa inayofanyika ya kupambania upatikanaji wa maji kwa wananchi wote wa Dar es Salaam na maeneo mengine.
Amesema kuwa kupitia ziara hii wamebaini sababu zilizosababisha upungufu wa maji mjini ikiwemo mvua kubwa zilizosababisha uharibifu wa miundombinu ya maji. Hivyo kwa sasa tunaweza kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi kupitia madiwani na wenyeviti wa mitaa kuhusu hali ya upatikanaji wa maji mjini.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa kazi ya maboresho kwenye mitambo ya kuzalisha maji imekamilika na sasa huduma imeimarika katika eneo la kihuduma kuanzia tangu siku ya jana.